Muhimbili kutumia njia ya kisasa kupandikiza meno ya kudumu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:50 PM Jul 31 2024
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko.

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, itaweka kambi maalum ya kupandikiza meno bandia, kwa njia ya kisasa kuanzia Septemba 2 hadi 6, mwaka huu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko, amesema hayo leo, kwamba kambi hiyo itahusisha madaktari bingwa, kwa kushirikiana na Bingwa wa Kinywa na Meno Mbobezi katika Upasuaji wa Taya, Dk. Chirag Desai kutoka Hospitali za Wockhardt nchini India.

Dk. Mfuko, alisema awali njia zilizokuwa zinatumika za kuweka meno bandia (Dentures), ni yale meno ambayo mtu anaweza kuweka kama ni jino moja au meno kadhaa, na kuyatoa, hivyo njia hii mpya itakuwa ni kuweka jino moja kwa moja na kulipandikiza kwenye mfupa wa taya.

‘’Faida za upandikizaji wa meno moja kwa moja kwenye mfupa wa taya ni kwamba yanakaa muda mrefu, hayawezi kutoka kirahisi, mtu ataweza kutafuna vizuri, kuongea vizuri na kumpa muoekano mzuri pia inampa kujiamini na kufurahia maisha kama ilivyokua awali,’’ ameongeza Dk. Mfuko

1

Alitoa rai kwa watu wote wanaosumbuliwa na changamoto ya meno kufika MNH-Mloganzila mapema kabla ya kambi hiyo kuanza, ili kufanyiwa vipimo na wataalam kisha kupatiwa huduma hiyo.

"Wenye changamoto ya meno wafike katika Kliniki yetu ya Afya ya Kinywa  na Meno, inayotoa huduma kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, saa tatu asubuhi hadi saa 10 jioni na kufanyiwa vipimo.

“Vipimo vya X-ray kuangalia mpangilio wa meno kwa sababu,  ili mtu aweze kupata huduma hiyo ni lazima afanyiwe vipimo mapema,” amesisitiza Dk. Mfuko.

2