KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amewapongeza Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Shinyanga, kwa utekelezaji wa miradi ya maji inayowanufaisha wananchi wa vijijini.
Ussi ametoa pongezi hizo jana Agosti 4, 2025, wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji maji katika vijiji vya Chona, Ubagwe na Bukomela vilivyopo katika Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.
"Rais Samia alivyoingia madarakani aliahidi kutekeleza miradi ya maji hadi vijijini. Leo tunaona utekelezaji huo kwa vitendo. RUWASA nawapongeza sana, mmemheshimisha Rais," amesema Ussi.
Aidha, amesema baada ya kukagua mradi huo kwa kina na kupitia nyaraka zake zote, wamejiridhisha kuwa umezingatia vigezo vyote vya utekelezaji na kwamba hauna dosari, hivyo Mwenge wa Uhuru umeridhia kuuzindua rasmi.
Amempongeza pia Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela na timu yake mgazi ya wilaya kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Februari 14, 2024 na kukamilika Julai 28, 2025, ambapo chanzo cha maji ni visima virefu vitatu vilivyochimbwa katika vijiji husika kwa gharama ya Sh. bilioni 1.4.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bukomela, wamesema mradi huo umewaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, na sasa wanatumia maji safi kwa shughuli za kila siku.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED