Wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo wametakiwa kuachana na tabia ya kutoa tiba kiholela kwa wanyama na badala yake kujenga utaratibu wa kupima mifugo ili kubaini aina ya ugonjwa kabla ya kuanza matibabu.
Wito huo umetolewa na Daktari wa Mifugo na Mtafiti Mkuu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dk. Donald Benju, wakati wa Maonesho ya Wakulima ya Nanenane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Dk. Benju amesema kuwa mazoea ya kuwapatia wanyama dawa kwa kubahatisha kwa kutegemea dalili za juu bila vipimo, yamesababisha mifugo mingi kupotea kutokana na matibabu yasiyo sahihi.
“Wafugaji wengi wanatoa dawa kwa mazoea bila kujua ugonjwa halisi unaomsumbua mnyama hii imekuwa chanzo kikuu cha vifo vya mifugo, kupoteza uzalishaji, na kuongezeka kwa gharama za matibabu zisizo na tija,” alisema.
Ameeleza kuwa lengo la ushiriki wa TVLA kwenye maonesho hayo ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya vipimo kabla ya kutoa dawa, sawa na ilivyo kwa binadamu.
“Mnyama anaponyesha dalili za ugonjwa, anatakiwa kupimwa kwanza ili kubaini tatizo lake halisi hii inasaidia kutumia dawa sahihi na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutumia dawa isiyo stahiki,” alifafanua.
Dk. Benju aliongeza kuwa matumizi ya maabara katika utambuzi wa magonjwa ya mifugo ni hatua muhimu ya kitaalamu, lakini bado ni jambo linalopuuzwa na wafugaji wengi kutokana na mazoea ya miaka mingi ya tiba bila vipimo.
Alionya kuwa utoaji wa dawa kiholela unaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na vifo vya mifugo, kwa sababu dawa inaweza kusababisha athari kali iwapo haitoshi au haifai kwa ugonjwa husika aidha, dawa zinazotolewa pasipo sababu huongeza msongo kwa mnyama na wakati mwingine haziwezi kusaidia hata kidogo.
“Matibabu holela yanasababisha pia usugu wa dawa. Unapotoa dawa isiyo sahihi mara kwa mara, vimelea vya magonjwa vinajifunza kuhimili dawa hizo hili linaweza kufanya matibabu kuwa magumu zaidi pale mnyama anapougua kwa kweli na kuhitaji dawa hiyo ambayo tayari imekwisha tumika vibaya,” alisema.
Ametoa wito kwa wafugaji kuitumia huduma zinazotolewa na TVLA, ambako sampuli kutoka kwa mifugo hukusanywa, kuchakatwa maabara, na hatimaye mmiliki wa mifugo hupewa matokeo pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu dawa inayopaswa kutumika.
“Huduma zetu hazijishii kwenye vipimo tu. Tunajihusisha pia na uchunguzi wa magonjwa ya wanyama, uzalishaji na usambazaji wa chanjo, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, usajili wa viuatilifu na utoaji wa mafunzo kwa wadau mbalimbali,” aliongeza.
Amesema hadi sasa, taasisi hiyo imezalisha takribani aina saba za chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mifugo, ikiwemo homa ya mapafu kwa ng’ombe, mdondo (kideri), kimeta, chambavu, homa ya mapafu kwa mbuzi,kitupa mimba na chanjo dhidi ya kitupa mimba.
Dk. Benju alitoa wito kwa wananchi kutembelea banda la TVLA katika maonesho hayo ili kupata elimu ya kina kuhusu mbinu bora za utambuzi, udhibiti na kinga dhidi ya magonjwa ya mifugo kwa lengo la kukuza afya na uzalishaji wenye tija.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED