MCHAKATO wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 umeendelea kuchukua sura ya kipekee katika maeneo mbalimbali nchini, ukibeba ushindani mkali, vilio, nderemo na mabadiliko makubwa ya kisiasa.
Zoezi hilo limetoa taswira mpya ya hali ya kisiasa ndani ya chama hicho tawala, huku baadhi ya vigogo na viongozi waandamizi wakiangushwa na sura mpya zikijitokeza kwa kishindo.
Katika mikoa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Zanzibar, Shinyanga, Tabora, Mara na Kigoma, kura za maoni zimeibua matokeo yaliyoshangaza wengi. Mawaziri, naibu mawaziri, wabunge wanaomaliza muda wao na viongozi wa kitaifa wa chama wamejikuta wakipoteza nafasi mbele ya wanachama wapya waliovuna kura nyingi, ikiwa ni ishara ya mabadiliko yanayotafutwa ndani ya chama.
Licha ya changamoto kadhaa kama kuchelewa kwa vifaa, makosa ya majina na migogoro ya kiuongozi katika ngazi za kata, mchakato huo umeendelea kwa hali ya utulivu na kushika kasi, huku ukifuatiliwa kwa karibu na wananchi, wachambuzi wa siasa, na vyombo vya habari kote nchini.
Ni matokeo yanayoashiria taswira mpya ya uongozi unaotakiwa na wanachama wa CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
USHETU
Katika hali isiyo ya kawaida, zoezi la kura za maoni ndani ya CCM katika kata za Ubagwe, Mapamba na Bulungwa, Jimbo la Ushetu, mkoani Shinyanga, lililazimika kuahirishwa juzi hadi jana baada ya watiania kugomea mchakato huo.
Sababu kuu iliyotajwa ni kukosekana kwa imani kwa makatibu wa kata waliodaiwa kukwamisha majina ya baadhi ya wagombea kutowasilishwa kwenye vikao vya juu vya chama.
Hata hivyo, uchaguzi huo uliohusisha zaidi ya wajumbe 1,000 uliendelea jana bila athari katika matokeo ya kura za ubunge, ambapo Emmanuel Cherehani aliibuka mshindi kwa kura 5,656, akifuatiwa na Mussa Misungwi (452), Machibya Mwabilija (171) na Valelia Mwampashe (153).
KAHAMA
Katika Jimbo la Kahama Mjini, Swerbet Nkuba alipata kura 1,389, huku Benjamini Ngaiwa aking'ara kwa kura 2,093 na kumwangusha pia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jumanne Kishimba (1,144). Wagombea wengine ni Francis Mihayo (821), David Kilala (191) na James Lembeli (219).
MSALALA
Mabula Magangila ameibuka mshindi kwa kura 5,518, akifuatwa na Ezekiel Maige (791), Ramadhani Shigaza (105) na Simon James (189).
SHINYANGA MJINI
Katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi anayetetea nafasi yake, amepata kura 2,922 akiwaacha mbali Stephen Masele (874), Paul Brand (34), Aboubakar Mukadamu (25), Hassan Fatihu (25), Hosea Karume (16) na Eustard Ngatale (10).
MKOA WA KAGERA
Katika Jimbo la Bukoba Vijijini, Dk. Jasson Rweikiza, anayetetea nafasi yake, ameongoza kwa kura 6,485, akifuatiwa na Falis Buruhan (4,619), Fahami Juma (239), Asted Mpita (124), Edimund Emmanuel (89) na Philibert Bagenda (44).
Jimboni Missenyi, Florent Kyombo ana matumaini ya kuteta nafasi yake baada ya kupata kura 2,979 akifuatwa na Projestus Tegamaisho (1,355) na Assumpta Mshama (475).
Khalid Nsekela amepata kura 5,693, akimwangusha Innocent Bilakwate (1,567) kwa Jimbo la Kyerwa.
Kwa Jimbo la Ngara, Msimamizi wa Uchaguzi, Mariam Amiry alimtangaza Dotto Bahemu kuongoza katika kura za maoni akiwa na kura 6,855 akifuatiwa na Stephen Kagaigai aliyepigiwa kura 2,344.
MKOA WA MARA
Katika Jimbo la Serengeti, Mary Daniel ameongoza kura za maoni baada ya kupata kura 11,533, akimwangusha Dk. Stephen Kebwe (2,903). Wengine na kura zao katika mabano ni Dk. Amsabi Jeremiah (1,400), Peter Mahende (1,029), Deogratius Chacha (489), Paulo King'embe (214). Mary ameweka rekodi kwa mwanamke wa kwanza kushinda kura za maoni jimboni humo.
Aidha, Robert Maboto anayetetea ubunge wake, ameongoza kura za maoni jimboni Bunda Mjini baada ya kupata kura 2,545, akifuatwa na Kambarage Wasira (2,032) na Ester Bulaya (625).
Mgore Miraji amepigira kura 2,255 kwa Jimbo la Musoma Mjini, akiwazidi kete Juma Mokili (1,543), Dk. Eliud Esseko (115), John Bwana (43), Philbert Sasita (34) na Mashaka Biswalo (44).
Wilayani Tarime, wabunge watatu waliokuwa wakitetea nafasi hizo, Mwita Waitara (Tarime Vijijini), Michael Kembaki (Tarime Mjini) na Jafari Chege (Rorya) wametetea nafasi zao.
KIGOMA MJINI
Shabani Ng’enda amepata kura 2,168 katika safari ya kutetea ubunge wake, akiwabwaga watangazaji Clayton Chipando 'Baba Levo'( 2,080) na Baruani Muhuza (264). Kuliibuka mvutano wakati wa utangazaji matokeo hayo, Baba Levo akitaka kura zihesabiwe upya kwa kuwa anaamini ameongoza.
VIGOGO 10 TABORA
Katika Mkoa wa Tabora mchakato umefanyika kwa amani na utulivu katika wilaya zote mkoani humo. Kati ya majimbo yote 12 ya ubunge mkoani humo, ni mawili tu ambayo wabunge wanaomaliza muda wao wamepata ushindi katika hatua hii ya kura za maoni, wengine wote wamepigwa.
Wabunge waliopenya katika hatua hiyo ni Magreth Sitta (Urambo) na Hussein Bashe (Nzega Mjini), huku majimbo 10 yaliyobaki walioshinda kura za maoni ni damu mpya.
Walioibuka kidedea katika jimbo la kura ni Shabani Mrutu (Tabora Mjini), Shaffin Sumar (Uyui), Munde Tamwe (Sikonge), Denis Kilatu (Kaliua) na John Luhende (Bukene).
Kwa upande wa Nzega Vijijini aliyepata kura nyingi ni Neto Kapalata, Abubakar Omari (Manonga), Henry Kabeho (Igunga Mjini), Juma Kawambwa (Igalula) na Japhael Lufungija (Ulyankulu-Kaliua).
MKOA WA ARUSHA
Mbunge wa zamani wa Arumeru Mashariki kupitia CHADEMA, Joshua Nassari, ameongoza katika kura za maoni za kiti cha ubunge, akipata kura 6,678, huku akimbwaga mbunge aliyemaliza muda wake, Dk. John Pallangyo aliyepata kura 652.
Fredrick Lowassa ambaye anawania kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili katika Jimbo la Monduli, ameshinda kura za maoni za kiti hicho baada ya kuongoza kwa kura 7,137.
Katibu wa CCM, Wilaya ya Monduli, Rukia Mbasha, alisema wagombea wengine, ni Isack Copriano, Mwenyekiti wa zamani wa Halmashauri hiyo, aliyepata kura 2,206, Wilson Kurambe (952), Shaban Adam (251), Bilihuda Kisaka (41) na Sakaya Alaisherio (21).
Jimboni Longido, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, ameshinda kwa asilimia 77.5 katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za ubunge, baada ya kuongoza kwa kura 9,064.
Dk. Kiruswa anafuatiwa na mpinzani wake, Petro Ngarikon aliyepata kura 1,421 sawa na asilimia 12.1, Nicolous Senteu (1,128) na Martha Ntopo (87).
Mbunge aliyemaliza muda wake Karatu, Daniel Awaki, ameongoza baada ya kupata ushindi wa kura 7,884, Cecilia Paresso akimfuatia kwa kura 1,341.
KILIMANJARO
Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA), Ngwaru Maghembe, ameshinda kura za maoni za ubunge katika jimbo la Mwanga, baada ya kupata kura 4,108.
Ngwaru amemwangusha mbunge aliyekuwa akiwania awamu ya pili, Wakili Joseph Thadayo, aliyepata kura 1,689.
Aliyekuwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ameibuka kidedea kwa kupata 3,029.
Katibu wa CCM, Wilaya ya Same, Amos Kusakula, alisema Anne anafuatiwa na Miryam Mjema aliyepata kura 1,763.
Mbunge aliyeliongoza kwa vipindi mitatu Jimbo la Same Magharibi, Dk. Mathayo David, ameibuka tena mshindi wa kura za maoni, kwa kupata kura 5,093, akifuatiwa na Fatuma Kange aliyepata kura 875.
*Imeandaliwa na Godfrey Mushi (ARUSHA), Samson Chacha (TARIME), Judith Julius (NGARA), Benny Kingson (TABORA), Vitus Audax (MWANZA), Shaban Njia (KAHAMA), Marco Maduhu (SHINYANGA)
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED