WACHEZAJI wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wameahidi kuwapa tena furaha Watanzania kwa kupata ushindi leo dhidi ya Mauritania, ukiwa ni mchezo wao wa pili wa Kundi B wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza soka la Ndani (CHAN).
Wakizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzao kuelekea mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, majira ya saa 2:00 usiku, mabeki Dickson Job na Shomari Kapombe, wamewataka mashabiki wa soka wa nchini kujitokeza kwa wingi uwanjani, wakiwaahidi kuwa hawatorejea nyumbani kinyonge.
Stars itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso, mchezo uliopigwa, Jumamosi iliyopita, katika mchezo wa ufunguzi wa fainali hizo.
"Mandalizi yamekamilika, sisi wachezaji na benchi la ufundi tumejipanga kwa ajili ya mchezo mgumu, lakini ni muhimu kwetu kupata matokeo ya ushindi.
"Sisi wachezaji tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunashinda mechi hii, tunawaomba tu Watanzania wenzetu wajitokeze kwa wingi kama ulivyokuwa mchezo wa kwanza na sisi tunawaahidi hawatotoka uwanjani kinyonge, tutahakikisha wanatoka na furaha kifua mbele," alisema Job, beki wa kati wa Taifa Stars.
Naye, beki wa kulia wa timu hiyo, Kapombe, alisema ushindi wa mechi ya leo utawapa mwanga wa kuelekea hatua inayofuata ya robo fainali, hivyo watakuwa makini kuhakikisha wanafanya vema ingawa mchezo utakuwa mgumu.
"Mwalimu amerekebisha makosa yaliyoonekana kwenye mchezo uliopita, tunatakiwa tufanye vizuri zaidi ya kile tulichokifanya kwenye mchezo uliopita, maadalizi yalikwenda vizuri sana.
"Mchezo huu ni muhimu zaidi, ndiyo ambao utatupa mwanga kuelekea kwenye hatua inayofuata ya robo fainali. Nawaomba Watanzania wanaoishi Dar es Salaam na wale wa mikoa ambayo iko jirani kuweza kujitokeza kwa wingi kuendelea kutupa sapoti kama walivyokuja kwenye mchezo wa kwanza, tunahitaji tena nguvu kama zile ili kutupa hamasa," alisema.
Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', yeye alisema amekiandaa vema kikosi chake na hasa eneo ambalo lilikuwa na changamoto ya umaliziaji.
"Kama nilivyosema timu yetu haina matatizo sana eneo la ulinzi, changamoto ipo kwenye umaliziaji, hilo ndilo eneo ambalo tulikuwa tunalitilia mkazo, hasa kuzitumia nafasi zinazopatikana, ilionekana kwenye mchezo wa kwanza," alisema kocha huyo.
Stars ambayo inaongoza Kundi B, ikiwa na pointi tatu, inahitaji ushindi ili kujiweka vema kutinga hatua ya robo fainali ya CHAN, ambayo inachezwa kwenye nchi tatu, Tanzania, Kenya na Uganda, ikiwa na vituo vinne, Dar es Salaam, Zanzibar, Nairobi (Kenya) na Kampala (Uganda).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED