Wabunge watano waanguka kwenye kura za maoni Singida

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:48 AM Aug 06 2025
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela
Picha: Mtandao
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela

MCHAKATO wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaendelea kuacha historia baada ya wabunge watano kati ya wanane waliomaliza muda wao mkoani Singida kuangushwa katika kinyang'anyiro hicho, huku mmoja akianguka mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na makatibu wa CCM wa wilaya mbalimbali, waliopoteza nafasi ni Ramadhani Ighondo (Ilongero), Musa Sima (Singida Mjini), Miraji Mtaturu (Ikungi Mashariki), Francis Mtinga (Iramba Mashariki) na Yahaya Masare (Itigi). 

Waliotetea nafasi zao na kuibuka na ushindi ni Dk. Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi), Dk. Pius Chaya (Manyoni) na Elibariki Kingu (Ikungi Magharibi).

 SINGIDA MJINI 

Yagi Kiaratu ameibuka na ushindi kwa kura 2,575, akifuatiwa na Khalid Ngulume (1,146). Mbunge aliyemaliza muda wake, Musa Sima amepata kura 678.

IRAMBA MASHARIKI

Jimboni Iramba Mashariki, Jesca Kishoa aliyekuwa miongoni mwa wabunge 19 waliofukuzwa CHADEMA baada ya kuapishwa kuwa wabunge nje ya ukumbi wa Bunge, ameongoza kwa kura 5,946, akimshinda aliyekuwa mbunge, Francis Mtinga (2,932).

ILONGERO

Katika Jimbo la Ilongero, mfanyabiashara Haiderali Gulamali ameongoza kwa kura 5,024, akiwashinda Lazaro Nyalandu (3,637) na Ramadhani Ighondo (2,922).

IKUNGI MASHARIKI

Jimboni Ikungi Mashariki, Thomas Kitima ameshinda kwa kura 2,100, akimwangusha mbunge aliyekuwa anatetea nafasi, Miraji Mtaturu (1,111).

IRAMBA MAGHARIBI

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba ameendelea kutamba katika jimbo hilo, akipata kura 10,604 dhidi ya wapinzani wake.

ITIGI, MANYONI

Katika Jimbo la Itigi, Yohana Msita alimshinda aliyekuwa mbunge, Yahaya Massare huku jimboni Manyoni na Ikungi Magharibi, Dk. Pius Chaya na Elibariki Kingu walifanikiwa kutetea nafasi zao.

MKOA WA DODOMA

Katika Mkoa wa Dodoma, aliyekuwa mbunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa ameangushwa na Mariam Ditopile, aliyepata kura 1,869. 

Jimbo la Kongwa, Spika aliyejiuzulu Job Ndugai ameongoza kwa kura 5,692, huku Mawaziri Dk. Ashatu Kijaji (Kondoa) na Anthony Mavunde (Mtumba) wakitamba katika majimbo yao.

Wagombea wengine waliopata ushindi mkubwa ni Kunti Majala (Chemba), George Simbachawene (Kibakwe), Samwel Malecela (Dodoma Mjini), Livingstone Lusinde (Mvumi) na Deogratius Ndejembi (Chamwino).

DAR ES SALAAM

Katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke, Daniel Sayi, amemtangaza Mariam Kisangi mshindi wa Jimbo la Temeke kwa kura 2,367 (sawa na asilimia 55), akifuatiwa na Fadhiri Mohamed aliyepata 1,389. Jasdeep Singh (959), mwanahabari Shafi Dauda (887), Bernald Mwakyembe (769), Doroth Kilave (288), Mussa Mtulya (60) na Leah Mwampishi (48).

Kwa Jimbo la Chamazi, Abdallah Chaurembo ameibuka kidedea kwa kura 2,765 (82%), akifuatiwa na Melkzedeck Hango aliyepata 391.

Jimbo la Mbagala, Kakulu Kakulu amepata ushindi wa kura 2,364, akifuatiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Issa Mangungu, aliyepata kura 795.

Katika Jimbo la Kibamba, Katibu wa CCM Wilaya ya Ubungo, Henry Mwenge, alimtangaza Angela Kairuki kuwa mshindi kwa kupata kura 4,655, akimshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Issa Mtemvu, aliyepata 615. 

MAWAZIRI WAANGUKA

Baadhi ya mawaziri, naibu mawaziri na viongozi waandamizi wa CCM Zanzibar wameanguka kwenye kura za maoni za kuwania nafasi za ubunge na uwakilishi, huku baadhi ya wateule wa Rais na vigogo wapya wakipeta kwa ushindi mkubwa.

Uchaguzi huo wa kura za maoni ulifanyika juzi kwa amani na utulivu katika majimbo mbalimbali ya Zanzibar, licha ya changamoto ya kuchelewa kuanza kwa upigaji kura katika baadhi ya maeneo, hususan Wilaya ya Magharibi B Unguja. Hali hiyo ilisababisha matokeo ya baadhi ya majimbo kutolewa hadi usiku wa manani.

Miongoni mwa waliokatwa na wanachama wa CCM ni: Shamata Shaame Khamis, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, aliyegombea uwakilishi Jimbo la Micheweni.

Juma Makungu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, aliyegombea uwakilishi Jimbo la Kijini.

Nadil Abdul-latif, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (aliyegombea uwakilishi Jimbo la Chaani).

Nassor Salim Jazira, aliyegombea uwakilishi Jimbo la Kikwajuni, Zubeda Khamis Shaibu, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mfenesini, na Abdulghafar Idrisa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtoni.

Wengine ni Mwantakaje Khamis, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bububu, Mtumwa Peya, aliyegombea uwakilishi Jimbo la Bubwini na Muhammed Ahmada, aliyegombea uwakilishi Jimbo la Malindi.

Wateule wa Rais waliogombea na kushinda ni: Ayoub Mohammed Mahmoud, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja (ameshinda kura za maoni ubunge wa Chaani) na Sadifa Juma Khamis, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A (ameongoza kura za maoni ubunge wa Donge).

Hamid Seif Said, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini, ameanguka katika mchakato wa uwakilishi Jimbo la Bubwini.

MOROGORO

Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Nuru John alisema upigaji kura kwa jimbo hilo uliahirishwa hadi jana katika Jimbo la Mikumi, baada ya kubainika kuwa karatasi za kupigia kura za ubunge na udiwani zilikuwa na makosa ya majina.

"Hatutaweza kutangaza matokeo ya Jimbo la Mikumi kwa sasa hadi kura katika kata ya Tindiga zipigwe tena baada ya kurekebisha makosa yaliyobainika," alisema.

Pia alieleza kuwa katika kata ya Mikese, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, wajumbe hawakupiga kura kutokana na makosa ya majina kwenye karatasi za kura za udiwani, na mchakato huo ulitarajiwa kufanyika jana.

Katika Jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga alipata kura 4,964 katika safari yake ya kutetea ubunge, akifuatiwa na Issa Vitus Lipagila (825), Aloyce Tendwa (344), Abdulla Lyana (283) na Denis Bandisa (118).

Jimboni Mvomero, Jonas Van Zeeland alipata kura 3,378 na kuweka matumaini ya kutetea nafasi yake, akifuatiwa na Suleiman Murad (3,261) na Sara Ally (1,638).

Kwa Jimbo la Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi anayetetea ubunge wake, ameongoza kwa kuwa 9,255, akifuatiwa na Dk. Ford Chisongela (809) na Menance Mhombwe (777).

Jimbo la Ulanga, Salim Hasham, anayetetea nafasi yake, amepata kura 4,622 dhidi ya Abdallah Kirungu (2,858) na Thabiti Dokodoko (565).

Ahmed Shabiby ameendelea kutamba katika Jimbo la Gairo kwa kura 9,198 akifuatiwa na Baby Brighton (393), Reuben Mwegoha (292) na Danstan Mziwanda (269).

Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Shabani Tale (Babu Tale) amepata kura 5,318 katika kutetea kiti chake, akifuatiwa na Omary Mgumba (1,310) na Robart Selasela (845).

Katika Jimbo la Morogoro Kusini, Zuberi Mfaume amepata kura 4,438, akiwafunika Mathew Mtigumwe (1,122), Adrian Jungu (666) na Dk. Suzanne Kibozi (641).

Jimbo la Mlimba, Dk. Kellen Rwakatare ameongoza kwa kura 4,029 dhidi ya Acley Mhenga (1,005) na Andrew Alyamuhindi (536).

Abdulaziz Abood ameendelea kutamba Morogoro Mjini, akipigiwa kura 4,311 dhidi ya Dk. Ally Simba (1,886) na Robert Kadikilo (131).

Jimbo la Malinyi, Dk. Mecktrids Mdaku amepata kura 2,450 na kumwangusha Antipas Mgungusi (1,408), aliyekuwa mbunge.