Watanzania wameendelea kuhamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Rai hiyo imetolewa jana Agosti 5, 2025 na Mjumbe wa Bodi wa Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Sophia Mgonja wakati wa hafla ya ugawaji wa majiko ya gesi ya kilogram 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Morogoro akiwa pia ameambatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Wakili Mwantumu Sultan.
“Nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na kampeni hii ya nishati safi ya kupikia ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kutunza mazingira.
Lakini pia tumpongeze Rais kwa kusimamia kampeni hii kwa vitendo kwa kutoa fedha zilizowezesha baadhi ya taasisi za kiserikali kama Jeshi la Magereza kuhama kutoka kutumia kuni na mkaa kupikia na kufungiwa mifumo ya nishati safi ya kupikia. Na leo Mhe. Rais ameona ipo haja na watumishi wa jeshi hili pia kutumia nishati safi ya kupikia na ndio maana tuko hapa kuwapatia majiko haya yanayotolewa na bure na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA),” amesema Mhandisi Mgonja.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Magereza, Peter Anatory amesema kuwa majiko hayo ya gesi yatakwenda kuwa motisha kwa watumishi wa jeshi hilo na kuahidi kuendelea kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka ili kutunza mazingira.
Kwa upande wake Mhandisi Godfrey Chibulunje ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa ugawaji wa majiko hayo ya gesi ni muendelezo wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na REA kuhakikisha maono ya Mhe Rais pamoja na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umebainisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia unafikiwa.
Awali akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 1166 yanagaiwa kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Morogoro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED