Ndumbaro, ahimiza kutokomeza ukatili kijinsia

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 07:18 PM Apr 09 2025
Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro
Picha: Hamida Kamchala
Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro

WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro, amewataka wananchi Mkoa wa Tanga, kuhakikisha wanashirikiana kutokomeza vitendo ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kutokana na takwimu kuonesha kwamba mkoa huo unaongoza kwa vitendo hivyo.

Ametoa wito huo, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) iliyofanyika jijini humo ambapo amesisitiza kila mmoja apambane kutokomeza vitendo hivyo.

Dk. Ndumbaro amebainisha kwamba, ili kutokomeza vitendo hivyo wananchi wote wanapaswa kushirikiana kuwabaini na kuwatia nguvuni wale wote watakaohusika kufanya vitendo hivyo bila kuoneana aibu au kuhofia kuvunjika kwa ujamaa au undugu.

"Vitendo vya ukatili wa jinsia vinaanzia kwenye familia, kwahiyo kila mmoja tuhakikishe tunaweka mkakati ya kutokomeza tatizo hili, na kila atakayefanya ukatili tusimuhifadhi, tumpeleke kwenye vyombo vya sheria akapate anachostahili" amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema wamepokea maelekezi na watahakikisha wanaendeleza kambi zitakazowekwa maeneo yote pamoja na kuwapatia wananchi huduma zinazostahili ili kupata haki zao.