MAZISHI ya aliyekuwa kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, yamefanyika jana nchini Italia na kuhudhuriwa na watu 200,000 kutoka mataifa tofauti.
Kabla ya kufanyika maziko, kulitanguliwa na ibada ya mazishi ya Papa Francis, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Viongozi wa serikali, wafalme, wanasiasa na watu maarufu ni miongoni mwa watu waliokusanyika katika viwanja vya Mtakatifu Petro, kushuhudia mazishi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki lenye waumini wengi duniani.
Katika jambo la kipekee mazishi hayo ya Papa Francis yamehudhuriwa na raia wa kawaida, wafungwa na wahamiaji ambao waliusindikiza mwili wake hadi kwenye kanisa ambako alizikwa.
Hata mazishi yake yalikuwa ya kawaida kwa kufuata wosia wake ambao ulieleza Papa Francis hakupenda mazishi ya kifahari.
Mapema asubuhi kengele za Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro zililia kuashiria kuanza kwa shughuli za mazishi ya Papa Francis ambapo uongozi wa Kanisa Katoliki ulisema zaidi ya watu 200,000 wamehudhuria misa hiyo ya mazishi.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni pamoja na marais wa nchi mbalimbali wakiwamo Donald Trump wa Marekani na mkewe Melania, Emmanuel Macron wa Ufaransa, Volodymyr Zelensky wa Ukraine na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Viongozi wengine ni Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya, Mwanamfalme William wa Uingereza na familia ya Kifalme ya Uhispania na wengineo wengi.
Maelfu ya waombolezaji walikusanyika kwenye barabara kuu inayofahamika kama della Conciliazione ambayo ndio inayoelekea kwenye Uwanja wa Vatican wa Mtakatifu Petro huku wakifuatilia misa kwenye televisheni kubwa zilizowekwa kwenye viwanja vya kanisa hilo.
Waombolezaji hao walipunga mikono kumuaga Papa Francis wakati jeneza lake lilopakiwa kwenye gari likipita barabara hiyo kuelekea katika kanisa la Mtakatifu Maria Maggiore, ambako mwili wake uliwekwa kaburini majira ya alasiri.
Kardinali mzee zaidi aongoza misa
Aliyeongoza ibada ya mazishi alikuwa Dekano wa Chuo cha Makadinali, Kardinali Giovanni Battista Re.
Kardinali huyo Muitaliano mwenye umri wa miaka 91 alipata upadrisho katika Jimbo la Brescia mwaka 1957 na Mwaka 2001, Papa John Paul II alimteua kuwa kardinali.
Kardinali Re alichaguliwa kuwa dekano wa Chuo cha Makadinali mwaka 2020, na Papa Francis aliongeza muda wake katika wadhifa huo mwezi Februari mwaka huu. Alishiriki katika mkutano mkuu wa makadinali wa Aprili 2005, ambao ulimchagua Papa Benedict XVI, na pia katika mkutano mkuu wa Machi 2013, ambao ulimchagua Papa Francis.
Kardinali Giovanni Battista Re alitoa risala ambayo inakumbuka maisha na urithi wa Papa Francis.
Wakati akitoa risala hiyo, kardinali alisema: upendo mwingi ambao wameushuhudia katika siku za hivi karibuni kufuatia kifo chake kwenda katika maisha ya milele unawakumbusha ni kwa kiasi gani utumishi mkuu wa Papa Francis uligusa akili na mioyo ya watu.
Aliwataka pia waombolezaji kujiepusha na vitendo vya kupeperusha bendera au mabango wakati wa ibada ya misa ya kumuaga Papa Francis.
Akumbukwa kwa kupenda amani
Akiwa mbele ya makardinali waliovalia mavazi yao mekundu, Kadinali Giovanni Battista Re alimuelezea Papa Francis kama papa wa watu, mwenye moyo safi na aliyehimiza amani.
Pia alimtaja Papa kama kiongozi aliyependa kushirikiana na jamii iliyotengwa, kuwasiliana na moja kwa moja na watu binafsi, aliyekuwa na shauku ya kuwa karibu na kila mtu na hasa waliokuwa na shida.
Alikumbushia falsafa ya Papa Francis ya kuhimiza amani ikuhusu mazungumzo ya kina katika juhudi za kumaliza mizozo inayoendelea kote duniani.
Trump, Zelensky wateta Vatican
Kama ishara ya kumuenzi Papa, Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine walikutana na kufanya mazungumzo ndani ya kanisa la Mtakatifu Petro.
Rais Tump, alisema mazungumzo hayo aliyoyataja kuwa yenye tija yalihusu namna ya kumaliza mzozo unaondelea kati ya Russia na Ukraine.
Mkutano huo wa dharura ulifanyika baada ya viongozi hao kufokeana ndani ya Ikulu ya White House mwezi Februari mwaka huu.
Maofisa kutoka pande zote mbili walithibitisha mkutano huo ulifanyika,huku hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu mazungumzo hayo.
Rais Trump na Zelensky walihudhuria ibada hiyo ya mazishi pamoja na wakuu wengine wa nchi na wanafamilia za kifalme.
Mkutano wao unakuja siku moja baada ya Rais Trump kusema Russia na Ukraine wako karibu sana kufikia makubaliano, baada ya mazungumzo kati ya mjumbe wake Steve Witkoff na Rais wa Russia Vladimir Putin yaliyofanyika mjini Moscow juzi.
Steven Cheung, ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu ya White House, alisema maelezo zaidi kuhusu mkutano wa faragha wa jana kati ya Trump na Zelensky yatatolewa.
Viongozi hao walikwaruzana na kurushiana maneno katika mkutano wao Ikulu ya Marekani, na haikutarajiwa wangekutana ana kwa ana katika wiki za hivi karibuni
Afrika kutoa papa mpya?
Kuzikwa kwa Papa Francis kumefungua mchakato wa kumtafuta papa mpya, lakini waafrika wengi wana matumaini safari hii kiongozi huyo inawezekana akatoka katika bara hilo.
Macho ya waafrika wengi yapo kwa kardinali Peter Turkso kutoka Ghana, ambaye jina lake linaendelea kutajwa kama mrithi wa kiti hicho.
Mwaka 2010 Kadinali huyo aligonga vichwa vya habari baada ya kueleza hakuwa tayari kuwa baba mtakatifu na pengine kanisa katoliki halijakuwa tayari kumpokea papa mweusi.
Baada ya miaka kumi na mitano jina la Kadinali Tukson linasikika katika mitaa ya Vatican kama mmoja wa wanaodhaniwa kugombea na kurithi nafasi ya kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani.
Hata hivyo, endapo atatwaa taji hilo, kadinali Tukson atakuwa ni mtu wa pili kutoka Afrika baada ya Papa Victor I, ambaye alitoka Afrika ya kaskazini takribani miaka 2000 iliyopita.
Madhehebu ya katoliki kwa sasa yanaendelea kukua kwa kasi barani Afrika na takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 20 ya waumini bilioni 1.4 wanapatikana Afrika.
BBC, DW
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED