MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wafanyabiashara kutumia kikamilifu dawati maalumu la uwezeshaji biashara kwa maendeleo ya taifa, likilenga kusaidia kutatua changamoto kuongeza ufanisi wa biashara.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa dawati hilo, Mtanda amesisitiza umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa, akisema kuwa kila Mtanzania anapaswa kuchangia kulingana na uwezo wake.
Pia ameitaka TRA kuhakikisha dawati hilo linafika hadi ngazi ya wilaya ili kuwafikia wafanyabiashara wote.
“Kodi ni suala la kitaifa hatutaweza kuiendesha serikali bila kulipa kodi maendeleo tunayoyaona sasa kwa mfano, daraja la Kigongo Busisi lililozinduliwa hivi karibuni yote ni matokeo ya kodi tunazolipa sisi wenyewe,” amesema Mtanda.
Naye, Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Faustine Mdesa, amesema dawati hilo si kwa ajili ya kutoza kodi bali kutoa msaada, kusikiliza changamoto na kuboresha ushirikiano kati ya TRA na walipa kodi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Mwanza, Jacob Paul alisema kuwa dawati hilo ni neema kwao kwani limewapa matumaini mapya.
“Tumekuwa na kero nyingi bila sehemu rasmi ya kuziwasilisha sasa tumepata sehemu sahihi ya kusaidiwa, na tumeahidi kulitumia kikamilifu,” kupata suluhisho la changamoto zetu”alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED