REKODI YA GUINNESS; Panya shujaa wa Tanzania ampiku mwenziwe Magawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:35 PM Apr 05 2025
Ronin
Picha: BBC
Ronin

RONIN, ni panya kutoka Tanzania, amekuwa akifanya kazi katika Jimbo la Preah Vihear, kaskazini mwa nchi ya Cambodia. Amevunja rekodi ya dunia ya Guinness.

Panya huyo amevunja rekodi ya awali, iliyokuwa ikishikiliwa na panya Magawa, ambaye naye pia alitokea Tanzania, ambaye aligundua mabomu 71 ya ardhini.

Sasa Ronin, kwa zaidi ya miaka mitatu kazini amekwishagundua mabomu ya ardhini 109 na vifaa vingine hatari 15.

Ronin, ana miaka mitano, alizaliwa Agosti 13, 2019. Ni wa kiume, ameweka rekodi mpya ya dunia, kwa kuwa panya wa kwanza kufichua zaidi ya mabomu 100 ya kutegwa ardhini na mabaki mengine ya zana za kivita ambayo yangesababisha maafa.

Shirika la kutoa misaada ya kutegeua mabomu yaliyotegwa ardhini lenye makao nchini Ubelgiji, liitwalo APOPO, linasema panya huyo kutoka bara la Afrika, Tanzania, anaweza kuendelea na jukumu hilo la kugundua mabomu ya kutegwa ardhini kwa miaka mingine miwili.

"Mafanikio yake ya kipekee yamemfanya apate taji la Rekodi za Dunia za Guinness kwa kuwa panya aliyegundua mabomu mengi ya ardhini," imesema APOPO.

Ronin alizaliwa mkoani Morogoro, ameipiku rekodi ya awali, iliyokuwa ikishikiliwa na panya Magawa, wakati wa utumishi wake wa miaka mitano, kabla ya kustaafu mwaka 2021.

Magawa, alitunukiwa medali ya dhahabu kwa ushujaa kwa kugundua mabomu katika takribani mita za mraba 225,000 za ardhi, sawa na viwanja 42 vya mpira.

Magawa alikufa mwaka 2022. Taifa la Cambodia bado limejaa maelfu ya mabomu yaliyotegwa ardhini kufuatia miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyomalizika mwishoni mwa miaka ya tisini.

Nchini Tanzania shirika hilo la Apopo pia linatumia panya wa kunusa, ili kutambua watu wanaougua ugonjwa wa kifua Kikuu.

Vifo kutokana na migodi na silaha zilizotegwa ardhini hutokea mara kwa mara Cambodia na karibu vifo 20,000 vimetokea tangu 1979 na mara mbili ya idadi hiyo wamejeruhiwa.

Watoto wawili wa Cambodia waliuawa mwezi Februari, mwaka huu, wakati guruneti lililotegwa tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, lililopuka karibu na makazi yao kaskazini magharibi mwa mkoa wa Siem Reap.

BBC