WATENDAJI wa serikali wako njiapanda. Dunia inasubiri kuona hekima yao: Kulinda na kuendeleza Mbuga ya Wanyama Saadani; au kuendelea kuimega kwa kutoa vipande vyake kwa kampuni zilizothibitika kuwa na mwelekeo wa kuharibu mifumo yake ya ikolojia.
Hii ni mbuga ya taifa. Lakini kampuni ya kuchimba chumvi – Sea Salt Limited imemegewa kipande. Kampuni ya kuzalisha sukari – Bagamoyo Sugar Limited imemegewa pia. Mmegaji ni yuleyule – serikali ambayo ni mmiliki wa Mbuga ya Saadani.
Zogo limekuwapo kimyakimya na sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amelikoka upya katika ripoti yake ya mwaka 2020/21 ambamo anabainisha kuwa kampuni iitwayo Sea Salt Limited inachimba madini ndani ya mbuga kwa kutumia leseni Na. ML 05/92.
Sasa hekima inahitajika hapa: Mbuga ya Saadani haipaswi kuwa na mwingiliano wa shughuli zozote za binadamu kama uzalishaji chumvi au sukari. Lakini Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sea Salt Limited, Ajay Sengar anasema anataka kupanua uzalishaji. Anaomba kuongezwa eneo.
Nani abaki? Nani asogee mbali? Nani aondoke? Ni hekima tu inahitajika kwa kuwa sheria zilishatumika vibaya, ama kwa kutojua au kwa makusudi. Kila mmoja wa washindani anapeperusha karatasi inayoitwa LESENI.
Mwenye eneo kubwa na linalochukua hata jina la eneo lote, ni Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA) inayosimamia mbuga na yenyewe kusimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Katika ripoti yake, CAG anasema “shughuli za uchimbaji madini husababisha uchafuzi wa mazingira utokanao na kumwagika kwa mafuta yanayotumika kwenye mitambo, takaoevu, uchomaji taka ngumu, na kelele ndani ya hifadhi.
"Kwa maoni yangu, shughuli hizi zinahatarisha mfumo wa ikolojia ndani ya hifadhi na hivyo kusababisha kutokuwapo uhakika wa uendelevu wa Hifadhi ya Saadani.”
CAG anapendekeza TANAPA ishirikiane na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mamlaka zingine za serikali “kutathmini athari za uchimbaji madini katika mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Saadani na kuchukua hatua stahiki."
Saadani imezingirwa na halmashauri nne za wilaya za Bagamoyo na Chalinze mkoani Pwani; na Pangani na Handeni mkoani Tanga. Ina ukubwa wa kilomita za mraba 1,100.
Hii ni hifadhi yenye aina 60 za wanyama. Kuna nyani 2,170, nyati 928, turo 730, twiga 654 na tembo 359 (Sensa ya Wanyamapori 2022).
Kuna aina zaidi ya 270 za ndege wakiwamo ndege adimu wanaoitwa Sokoke Pipit, wenye rangi mchanganyiko na ambao hawapatikani sehemu nyingi duniani; na kuna mijusi, kenge na mamba katika mfumo wake wa ikolojia.
Hifadhi imebeba pia samaki, matumbawe – “vichaka-bahari” chini ya maji – ambako samaki hutaga mayai. Kwenye ufukwe wa hifadhi hii ndiko kwenye mchanga unaoitwa “mchanga wa fungani” – ule uachwapo maji yanapokupwa na ambamo kasa wa kijani hufukua na kutaga.
Uzuri na ubora wa Saadani siyo tu wanyama, wadudu na mandhari. Kuna mapato – uchumi. Mwaka 2021/22 peke yake, taifa liliingiza Sh. bilioni moja kutokana na watalii 28,355 waliotembelea mbuga hii.
Yanayoendelea Saadani hivi sasa, yanaibua kumbukumbu za mwaka 1959. Mjerumani aitwaye Bernhard Grzimek, mwanaharakati wa uhifadhi wa asili, alipoandika na kutengeneza filamu iitwayo, Serengeti Shall Not Die – Serengeti Haitakufa.
Ujumbe wa filamu ulilenga kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kulinda na kuhifadhi Mbuga ya Serengeti na thamani yake kiikolojia “kwa manufaa ya wakazi wa eneo husika na jamii za kimataifa.”
Nani leo ataandika na kutengeneza filamu ya Saadani Haifi? Na Saadani ni mali, ni fedha, ni ajira, ni kiburudisho kwa watu wa ndani na nje ya nchi. Ni uhai. Hatimaye, ni saadani – jema, zuri, hazina, msaada – tafsiri ambazo jina la mbuga limepewa katika lugha mbalimbali duniani.
Mwekezaji anayechimba chumvi alipewa na serikali leseni ya kuchimba madini kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 2,400. Kati ya hizo, ekari 728.17 zimeendelezwa bila kibali cha TANAPA, jambo ambalo CAG ameonesha ni kinyume cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Sura ya 123, Kifungu cha 95(1)(c).
Sheria inatamka kwamba mwenye leseni ya kuchimba madini, chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa ya Mwaka 1959, hatoendeleza ardhi ambayo ni mali ya TANAPA, mpaka apewe idhini na mamlaka hiyo.
Aidha, shughuli nyingine za kibinadamu ambazo zimetajwa kuharibu amani ya mbuga ni pamoja na mifugo – kama vile mbuzi, kuku, mbwa, mingurumo ya mitambo na kelele za binadamu.
Wafugaji mbugani ni miongoni mwa watumishi wapatao 100 katika kiwanda cha chumvi na wakazi wapatao 200 wa kitongoji cha Makupani kijijini Saadani ambako CAG anasisitiza kuwa “mifugo ina uwezekano wa kuambukiza magonjwa kwa wanyamapori.”
Mwandishi ameona barua ya tarehe 10 Mei 2021, yenye kumbukumbu Na. AB.2013/222/01/10 kutoka kwa Kamishna wa TANAPA kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Maudhui ya barua hii yanajenga shaka kuhusu ustawi wa Saadani kutokana na kuwapo shughuli za uchimbaji madini na kilimo ambazo si za kihifadhi wala rafiki kwa ikolojia yake.
Lakini ni miaka mitatu sasa, hakuna kilichofanyika kurekebisha hali katika mbuga ambayo umaarufu wake unapaa na mapato yake kwa taifa yanaongezeka; huku mazingira yake yakiendelea kutishiwa kiikolojia.
Zogo linalotishia kumega Saadani linafahamika kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Novemba 21, 2016 aliagiza kuwekwa alama za mipaka (bikoni) kwenye maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
Aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa SANAPA, Ephraim Mwangomo (amehamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere) anasema walitekeleza agizo la waziri mkuu, lakini walipofika eneo lenye mradi wa chumvi, walilazimika kuparuka kuweka bikoni kutokana na utata uliotajwa awali.
Anasema Kamati Teule ya Mawaziri Wanane ilizuru Saadani Oktoba 2019. Hata hivyo, mgogoro huo haujatatuliwa na wao wanasubiri kutekeleza kitakachoamuliwa na kamati.
Mwandishi pia alizungumza na Dk. Samuel Gwamaka, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Alikiri kuwa na taarifa za kinachoendelea kati ya SANAPA/TANAPA na mwekezaji wa mradi wa chumvi.
Anasema, "…miezi sita iliyopita nilikwenda kuangalia kinachoendelea; mwekezaji ameomba kuongezwa eneo ili kupanua mradi wake; lakini kuna shida… Tumeagiza kufanyike ukaguzi wa athari za mazingira ili hatua zichukuliwe. Ripoti ya ukaguzi huo ndiyo itakuwa mwongozo wa hatua za kuchukua…”
Makazi ya watu ndani ya mbuga yalianza miaka 48 iliyopita, pale Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lilipoanza uzalishaji chumvi na kuvuta watu wengi waliosaka ajira na kujenga vibanda kwa ajili ya makazi ya muda.
Kwa mujibu wa John Mbota (56), Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makupani, uliko mradi wa chumvi, makazi yalianza mwaka 1975 pale STAMICO ilipoanza uzalishaji chumvi na kuvutia uhamiaji wa watu waliosaka ajira, hata wakadumisha makazi.
Anasimulia kuwa eneo lenye mgogoro lilitolewa kwa STAMICO na Serikali ya Kijiji cha Saadani. Kufikia mwaka 1986 shirika lilikuwa limejenga kiwanda chake ambacho Mbota anakiri kilikuwa kivutio kwa watu wengi waliosaka ajira; na hatimaye wakalazimika kujenga vibanda ambavyo sasa vingi vimechakaa.
Anafafanua kuwa Kitongoji cha Makupani kawaida kina wakazi 200, lakini msimu wa kuvuna chumvi, idadi huongezeka hadi 800 au zaidi kutokana na shughuli za uvuvi na uvunaji chumvi.
“Changamoto kubwa kwa wakazi ni kuvamiwa na wanyamapori wakali, hasa chui na nyati. Miaka ya karibuni tumekuwa na shida ya chui kuja hapa kwenye makazi ya watu na kuchukua mbuzi. Pia kuna bughudha ya askari wa TANAPA wanapokuwa wakisaka wawindaji haramu,” anaeleza Mbota.
Ofisa Ardhi Halmashauari ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Deo Msilu anakubali kumwonesha mwandishi, nakala ya leseni ya uchimbaji madini Saadani iliyotolewa na Wizara ya Madini mwaka 1992 na kuhuishwa mwaka 2020; ikionesha ramani ya eneo la mradi inavyoingiliana na himaya ya SANAPA.
Msilu anasimulia kuwa eneo lenye mgogoro lilinunuliwa na Sea Salt Limited mwaka 1997 toka STAMICO. Kampuni ya uchimbaji chumvi ilisajiliwa nchini Septemba 4, 1998; na SANAPA ilianzishwa miaka saba baadaye kwa Tangazo la Serikali Na. 281 la tarehe 16 Septemba 2005.
Hata hivyo, kabla ya hapo, eneo hilo lilitengwa kama Pori la Akiba Saadani na kwa maana hiyo, lilikuwa na maslahi maalumu serikalini.
Hivi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze inapokea wastani wa Sh. milioni 32 kwa mwaka zikiwa ushuru wa huduma toka kampuni hiyo.
Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Gabriel Genda anasema kiwanda cha chumvi kimeingia ndani ya maeneo ya mbuga na kwamba ufafanuzi zaidi utatolewa na Kamati Teule ya Mawaziri Wanane inayoshughulikia mgogoro huo.
Mwandishi alipofika ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dodoma, kupata maelezo juu ya malalamiko hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele, alimshauri arudi Saadani ili apate maelezo kutoka kwa mtendaji mkuu wa hifadhi.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mwangomo alisema, wakati hifadhi inaanzishwa mwaka 2005, wakazi wa vijiji vya Saadani na Buyuni waliruhusiwa kuishi karibu na hifadhi “kwa sababu vilikuwapo kabla ya eneo hilo kutangazwa kuwa hifadhi ya taifa.
“Changamoto ni kwamba, ili uvifikie vijiji vya Saadani na Buyuni, lazima upite katika mbuga. Hakuna barabara wala njia nyingine ya mkato ya kwenda katika vijiji hivyo. Wakazi wake wanapita bila kulipia.
“Kwa hiyo, Sea Salt Limited imo eneo la STAMICO ambalo limo ndani ya kijiji cha Saadani, na ili ufike kwenye mradi wao, lazima upitie hifadhini,” alifafanua.
Kamishna Mwangomo alisema hifadhi imetoa kibali maalumu kwa magari ya mradi wa chumvi, “lakini wageni wao tunawatoza."
Alieleza kuwa baadhi ya maeneo, hususani uliko mradi huo wa chumvi na maeneo inakopita barabara hiyo, yameathirika, hasa kuhusu ustawi wa viumbe, na sasa yanahitaji kurejeshewa uhalisia.
"Eneo lenye chumvi, kwa maana inakochimbwa au ilikomwagika, majani hayaoti tena. Uliko mradi wa chumvi, kuna mikoko ambayo ni muhimu sana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Wao walikuwa wanaikata. Mikoko ina uwezo wa kufyonza hewa ukaa mara tano zaidi ya mimea mingine,” alieleza.
Kamishna Mwangomo alisema wamemwambia mwekezaji asikate mikoko, akisema: “Wao hawapendi mvua ili wavune chumvi nyingi; sisi tunataka mvua ili kuwe na majani zaidi hifadhini.”
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sea Salt Limited, Ajay Sengar anabainisha kiwanda chake kwa sasa kinazalisha asilimia 30 ya uwezo wake, kikiwa kimeajiri Watanzania 93 kati ya wafanyakazi wao 100 (wanawake 30); wakiingizia serikali dola za Marekani 100,000 kwa mwaka kutokana na tani 1,500 za chumvi wanazouza Kenya; kulipa ushuru halmashauri na gharama za TANAPA.
Ripoti ya Takwimu za Msingi Tanzania 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Juni 2022, inaonesha uzalishaji chumvi nchini mwaka 2021 ulikuwa tani 112,995. Hii ina maana kwamba, tani 1,500 za chumvi zinazopelekwa Kenya na Kampuni ya Sea Salt Limited ni sawa na asilimia 1.3 ya chumvi yote inayozalishwa nchini kwa mwaka.
Saadani ni hifadhi yenye mifumo mitatu ya kiikolojia; nchi kavu, bahari na mlango wa Mto Wami kwenye Bahari ya Hindi.
MAPATO YA SAADANI
Mwaka Watalii Mapato
2019/20 13,865 Mil. 682/-
2020/21 20,840 Mil. 734/-
2021/22 28,355 Bilioni 1/-
CHANZO: SANAPA, Machi 9, 2023.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED