Mgombea urais wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema mzigo wa matibabu kwa wagonjwa ambao serikali imeahidi kuubeba ni kwa wale wasio na uwezo tu.
Ahadi hiyo aliitoa Agosti 28, mwaka huu, wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika mkoani Dar es Salaam. Alisema endapo atapata ridhaa kuongoza nchi kwa mara nyingine, ndani ya siku 100 za awali, serikali itaanza kugharamia matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo kwa magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo saratani, moyo, sukari, figo, mifupa na mishipa ya moyo
Akizungumza leo Septemba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma, wilayani Momba, mkoani Songwe, akiendelea na kampeni kunadi sera na ilani ya chama hicho, Samia amesema:
“Wakati nikizindua kampeni za CCM Dar es Salaam, niliahidi bima ya afya kwa wote kuanza kufanyiwa kazi kwa majaribio.“Nilisema kuna magonjwa serikali itabeba mzigo, hii ni kwa wale wasio na uwezo. Maeneo mengine huko wanasema kwa kila Mtanzania.
“Nilisema ni kwa wale wasio na uwezo, ukidhibitika huna uwezo serikali itabeba mzigo wa matibabu, lengo ni kwa ajili ya ustawi wa watu wetu, wananchi waimarike , makusanyo yapatikane na nchi iendelee,” amefafanua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED