Jopo la mawakili wa Serikali limeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuzuia matangazo ya moja kwa moja (live streaming) ya mwenendo wa kesi ya uhaini dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, wakati mashahidi wa siri watakapokuwa wanatoa ushahidi.
Mawakili hao ni Nassoro Katuga (Wakili wa Serikali Mkuu), Tawabu Issa, Job Mrema, Mosie Kaima (Waandamizi), pamoja na Carbert Mbilingi na Winiwa Kasala (Mawakili wa Serikali).
Akiwasilisha hoja hiyo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga, Katuga alisema kuwa ingawa Mahakama Kuu imeruhusu mashahidi ambao ni raia kufichwa, kuna haja ya kuzuia matangazo mubashara wakati Lissu akisomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (committal proceedings).
Ameeleza kuwa kurusha matangazo katika hatua hiyo ni sawa na kuchapisha ushahidi, jambo ambalo litakuwa kinyume na amri ya Mahakama inayolenga kulinda usalama na utambulisho wa mashahidi hao.
“Kwa kuwa ushahidi huo utatolewa kwa namna ya siri, matangazo mubashara yanaweza kusababisha mashahidi kutambulika kupitia maelezo yao, hivyo kuhatarisha ulinzi wao,” amesema Katuga.
Amebainisha kuwa hawajaiomba kesi isikilizwe kwa siri, bali wanasimamia amri sita zilizotolewa na Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu kuhusu namna ya kulinda mashahidi.
Akijibu, Lissu alidai kuwa upande wa mashtaka unapanua tafsiri ya amri ya Jaji Mtembwa kwa kufunika mambo ambayo hayajakatazwa.
“Jaji alisema utambulisho wa mashahidi hautatolewa hadharani – majina, anuani zao wala mahali wanapokaa. Jamhuri wanachotakiwa kufanya ni kuchuja ushahidi kwa kuficha taarifa binafsi, si kuzuia matangazo mubashara,” alisema Lissu.
Ameeleza kuwa tayari taarifa binafsi za mashahidi zimeondolewa kwenye nyaraka, hivyo hakuna sababu ya kuzuia matangazo mubashara.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hadi Jumatatu, Agosti 18, 2025, kwa ajili ya kutoa amri ndogo na kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Lissu alitoa kauli za kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania, akisema miongoni mwa maneno:
“Tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi… huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED