Takukuru yanusa ufisadi mil 26/- ujenzi zahanati

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:24 PM Sep 03 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, imenusa harafu ya ufisadi baada ya kubaini Sh.milioni 26 zilizotolewa na serikali kupitia mfuko wa jimbo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Songambele wilayani Shinyanga, kukaa zaidi ya miezi mitatu bila kutumika.

Imeelezwa kuwa fedha hizo zilipitia kwenye akaunti ya Kituo cha Afya Salawe, ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo, lakini hazikutumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy, amebainisha hayo leo Septemba 3,2025 alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025 kupitia program ya Takukuru Rafiki.

Amesema wananchi wa Songambele walijitolea nguvu kazi kujenga zahanati hiyo kwa zaidi ya miaka 16, na  serikali ilitoa fedha hizo kupitia mfuko wa jimbo, lakini hazikutumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Amesema, walizifuatilia fedha hizo kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, na kuwekwa mikakati ya kutumika kuikamilisha Zahanati hiyo.

“fedha hizi zilitolewa kwenye akaunti ya Kituo cha Afya Salawe, na kutumika kufanya manunuzi ya vifaa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Songambele, na tulifanya ufuatiliaji vifaa vyote vilinunuliwa, na kuwezesha kukamilisha ujenzi wa Zahanati, na sasa wananchi wanapata huduma za matibabu,” amesema Kessy.

Katika hatua nyingine amesema, kwa kipindi hicho wamefanikiwa kuzuia mianya ya Rushwa kwenye miradi 11 ya maendeleo, yenye thamani ya sh.bilioni 3.5, baada ya kubaini kasoro ndogo ndogo ambazo zingesababisha miradi kujengwa chini ya kiwango na walitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho.