Upande wa Jamhuri watoa neno kesi ya Lissu

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:46 PM Apr 24 2025
Upande wa Jamhuri watoa neno kesi ya Lissu
Picha: Mtandao
Upande wa Jamhuri watoa neno kesi ya Lissu

Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kutoa amri kwa mshtakiwa huyo kufika mahakamani kwa njia ya mtandao ili kesi yake iendelee kusikilizwa.

Ombi hilo limetolewa leo Aprili 24, 2025 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwa njia ya video (video conference).

Wakili Mrema ameeleza kuwa ombi hilo limetokana na taarifa zilizotolewa na askari wa Magereza kutoka Gereza la Ukonga, kwamba mshtakiwa Lissu amekataa kuendelea kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao.

"Tunaomba Mahakama yako tukufu itoe amri rasmi kwa mshtakiwa kufika mbele ya Mahakama kwa njia ya mtandao katika tarehe nyingine kesi itakapopangwa kwa ajili ya kutajwa," amesema Mrema.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kuwa mnamo Aprili 3, 2025 ndani ya jiji la Dar es Salaam, Lissu alitoa kauli zenye lengo la kushawishi au kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu. Kauli hiyo ilinaswa katika video iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii ambapo Lissu alinukuliwa akisema:

"Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi... hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko... kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana."