INEC yatua Shinyanga mchakato ugawaji Jimbo la Solwa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:06 PM Apr 24 2025
Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk akizugumza kwenye kikao hicho.
Picha: Marco Maduhu
Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk akizugumza kwenye kikao hicho.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),imefika wilayani Shinyanga, kwa ajili ya kujiridhisha na kuhakikisha kama taratibu zote za kisheria zimezingatiwa katika mchakato wa kuligawa Jimbo la Solwa.

Ziara hiyo ya INEC imeambatana na kikao kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kikihusisha viongozi mbalimbali wa serikali na wawakilishi wa vyama vya siasa. 

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi wa Daftari la Wapiga Kura na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa INEC, Stanslaus Mwita, amesema wamefika mkoani humo kwa lengo la kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa maelekezo waliowahi kuyatoa kuhusu mgawanyo wa jimbo hilo. 

“INEC tumefika hapa wilayani Shinyanga kwa ajili ya kujiridhisha na kuhakikisha kama taratibu zote za kisheria zilifuatwa, hii ni hatua mojawapo ya mchakato wa kuligawa Jimbo la Solwa, na siyo kwamba tayari tumeridhia rasmi mgawanyo huo,” amesema Mwita.
Mkurugenzi wa Daftari la Wapiga Kura na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa INEC, Stanslaus Mwita, akizungumza kwenye kikao hicho.

  Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk, amesema awali baada ya kupokea ombi la kuligawa jimbo hilo,Tume ilifanya uchambuzi wa kina kwa kuzingatia vigezo vyote vya kisheria na kiutawala. 

“Tume imefika katika eneo husika kwa ajili ya tathmini ya mwisho, ili tuweze kuendelea na mchakato wa kuligawa jimbo la Solwa, na taarifa rasmi itatolewa juu ya kuligawa jimbo hili,” amesema Jaji Mbarouk.

 Nao baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho akiwamo Katibu wa Chadema Jimbo la Solwa Mashindike Bulaya, amesema jimbo hilo la Solwa linapaswa kugawanywa mara mbili sababu ni kubwa,na kwamba baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakikosa huduma muhimu kwa wakati. 

“Jimbo la Solwa ni kubwa mno. Kugawanywa kwake kutasaidia kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza uwakilishi bora,” amesema Bulaya. 

Aidha,iwapo Tume itaidhinisha rasmi mgawanyo wa Jimbo la Solwa,kutakuwa na  majimbo mawili ya uchaguzi, ambayo ni Jimbo la Solwa na Jimbo jipya la Itwangi.

Wadau