Wasira: Muungano ni nguzo ya umoja

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:20 PM Apr 24 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni tunu ya kipekee inayopaswa kulindwa na kuenziwa kwa nguvu zote kwa sababu ndio chimbuko la amani, mshikamano na maendeleo ya Taifa.

Pia Wasira ameeleza kuwa muungano huo ulioasisiwa Aprili 26, 1964, umejenga msingi wa taifa imara, lenye uwezo wa kupambana na changamoto za kiuchumi na kijamii kwa mshikamano. 

Wasira ameyaeleza hayo leo akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ilani mkoani Dodoma Wilaya ya Bahi 

katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia wa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.

“Muungano wetu si wa karatasi tu. Ni damu, ni historia, ni msingi wa umoja wetu. Bila Muungano huu, Tanzania isingekuwa na sura tuliyo nayo leo, ukivunjika itakuwa hasara kwa Bara na Zanzabar,” amesema Wasira.

1

Amebainisha kuwa kupitia muungano, Watanzania wamenufaika na taasisi za pamoja kama Jeshi la Ulinzi (JWTZ) Bunge la Jamhuri ya Muungano, pamoja na programu nyingi za maendeleo, zinazotekelezwa kwa faida ya pande zote mbili za muungano.

Amesema licha ya changamoto za hapa na pale, CCM itaendelea kusimamia muungano huo kwa nguvu zote kama dira ya kujenga Tanzania moja, yenye heshima na nafasi katika jukwaa la kimataifa.

“Nawaomba muendelee kuuenzi muungano huu. Tushikamane, tuulinde, tuuimarishe. Huu ndio urithi wetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” ameongeza.


Katika ziara hii inayoendelea, Wasira pia amekutana na viongozi wa chama ngazi ya wilaya na kata, akisisitiza nidhamu, mshikamano na uwajibikaji katika kutatua kero za wananchi.

2