JOWUTA: Wanasiasa msisimange waandishi wa habari

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:35 PM Apr 24 2025
Waandishi wahimizwa kufuata weledi
Picha: Christina Haule
Waandishi wahimizwa kufuata weledi

CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimewataka viongozi wa vyama vya kisiasa kuacha tabia ya kuwasimanga waandishi wa habari wakati wakitimiza majukumu yao.

Kimesema, wanataaluma hao waachwe huru, ili wafanye kazi bila mashinikizo na kutimiza malengo ya wananchi, kwa kufuata maadili na misingi ya kazi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Mussa Juma, ametoa wito huo wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha pamoja mkoani Morogoro Waandishi wa Habari kutoka mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro.

Waandishi wahimizwa kufuata weledi
Amesema mafunzo hayo lengo ni kuwajengea uwezo waandishi kuripoti uchaguzi mkuu kwa amani, kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa, usalama wao wenyewe kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Musa amesema viongozi wa vyama vya kisiasa wanapaswa kuwaacha wanahabari kufanya kazi kwa uhuru na kuacha kuwapiga na kuwazomea kwenye misafara.

Wanachama na viongozi wa JOWUTA
Hivyo amewahimiza wanahabari kuzingatia maadili na weledi katika utendaji wao wa kazi katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo, pasipo kuegemea chama chochote cha siasa.

“Tunataka waandishi wasiwe na upendeleo katika vyama vya siasa, watoe fursa sawa kwa vyama vyote kipindi chote cha uchaguzi, tumekutana kuwakumbusha pia suala la usalama wao wakati wa uchaguzi.

“Ili uchaguzi unapomalizika wabaki salama, jinsi gani wanaweza kujilinda na majanga mbalimbali, tumewaelekeza jinsi ya kujilinda na majanga ya mtandaoni,” amesema Mussa.

Mwandishi wa habari, Idda Mushi, amesema wanataaluma hao watimize wajibu wao ipasavyo katika kuandika habari zisizoleta sintofahamu kwa jamii, huku wakizingatia weledi katika utendaji wa majukumu.

“Ni jambo jema litakalosaidia kuzingatia kuwa kalamu ya mwandishi inauwezo mkubwa wa kusababisha uchochezi na vurugu kwenye uchaguzi zinazoweza kuleta machafuko nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Ofisa Uchaguzi Manispaa ya Morogoro, Shabani Duru, amewasisitiza waandishi wa habari kuwa na ushirikiano wa karibu na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), wakati wa kutekeleza majukumu yao kwenye mchakato mzima wa uchaguzi mkuu.