KWA kiumbe chochote, inatajwa kuwa mfumo wa fahamu unabeba hatua zote za kumwongoza katika taarifa na hata kujua mambo yake.
Mfumo huo hufanya kazi kwa kasi zaidi, mithili ya mfumo wa umeme, 'swichi' inapowashwa mara moja matokeo ni taa kuwaka.
Mfumo wa fahamu ulioundwa kwa neva na mishipa midogo kuanzia utosini hadi kwenye unyayo, hutoa taarifa papo hapo inapotokea chochote, kama ulivyo umeme.
Mathalani mtu amejichoma na mwiba, chupa, au kung'atwa na mdudu, taarifa husafirishwa mara moja, hadi kwenye neva ya fahamu, ikitoa ujumbe, hata kama hajakiona kwa macho hicho kitu. Taarifa itatambulisha ni kitu chenye ncha kali au la.
Mbali na manufaa ya mfumo huo, yako magonjwa kadhaa ambayo huukumba, kama ambavyo viungo vya mwili maeneo mengine pia huugua. Ugonjwa wa kutetemeka, humpata mwanadamu.
Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ubongo, Mishipa ya Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Brighton Mushengezi, akitoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa huo, hivi karibuni, Dar es Salaam ana ujumbe kuhusu ugonjwa huo.
Anasema ugonjwa wa kutetemeka huwakumba wenye umri wowote, hauchagui jinsia, ingawa hasa tatizo ni kwa watu wazima.
"Ugonjwa huu wanaugua wake kwa waume. Hasa wanaougua ugonjwa huu ni kuanzia umri wa miaka 40 na kuendelea, wapo wanaokuja wana tatizo wa umri mdogo, lakini ni wachache.
"Tatizo linaathiri zaidi vidole, mikono, sauti, kichwa, miguu vyote hutetemeka," anasema bingwa huyo.
Kadhalika, anasema ugonjwa huo chanzo chake kwa nusu asilimia haufahamiki sababu ingawa kwa asilimia 50 hutokana na jenetiki.
Mara kadhaa anasema ugonjwa huo dalili zinakuwa pale mtu akitaka kujihudumia kama vile kutaka kunyanyua kitu, kama kikombe, glasi au kufunga kamba za viatu, kuzungumza, hutetemeka.
"Pale mtu anapotakiwa kuwa makini kufanya kitu fulani, mfano hata anayetaka kumchoma sindano mgonjwa, utakuta akianza kile kitendo anaanza kutetemeka," anafafanua.
"Chanzo cha ugonjwa wa kutetemeka kwa asilimia 50 ya tatizo linahusisha jenetiki, wapo wanaoumwa ukiwauliza watakwambia walikuwamo wazazi au wanafamilia yao waliwahi kuugua ugonjwa huo," Dk. Mushengezi anasema.
Pia, anataja chanzo kingine kwa asilimia 50 hakifahamiki, ingawa kuna homoni mojawapo mwilini ya thyroid ikiwa juu husababisha.
Bingwa huyo, anaeleza namna ugonjwa wa kutetemeka anapoupata mtu, huwa ni wa kudumu na mgonjwa huhitaji matibabu ya muda mrefu.
"Huwa ni tatizo la kudumu kwa mtu, ingawa tiba ipo. Kwanza ni ‘ku-control' (kudhibiti), kutetemeka au kuondoa kabisa kutetemeka.
"Matibabu ni mgonjwa atapaswa kutumia dawa kwa muda wote maishani na anapoacha, tatizo hurejea tena," anasema bingwa huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED