Waraibu nao wahitaji haki kama za wenye TB, Ukimwi na malaria

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 06:00 PM Apr 24 2025
Wanaodaiwa kuwa ni watumiaji wa dawa za kulevya
Picha: Mtandao
Wanaodaiwa kuwa ni watumiaji wa dawa za kulevya

KATIKA dai la haki tiba nchini, waraibu wa dawa za kulevya, sasa wameibuka kitaalamu na kiutawala kupata haki tabibu za kitaifa.

Hoja yao wanataja kuwa ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini kuathirika na magonjwa sugu kama Homa ya Ini (Hepatitis), Ukimwi na Kifua Kikuu (TB). 

Hiyo inatokana na mustakabali wa maisha yao yalikosimama, sambamba na magonjwa hayo yanayotajwa kuenea kwa kasi miongoni mwao.

Sababu kuu inaelezwa kuangukia tabia hatarishi walio nayo, kama vile kutumia sindano kwa kuchangia, pia kuishi katika mazingira duni kiafya.

Inatajwa, Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupambana na janga hilo, huku waraibu hao wakihitaji huduma bora za kinga, matibabu na uangalizi wa kiafya.

Kutokana na hali hiyo, waraibu hao wanatoa wito kwa Mfuko wa Kimataifa uitwao Global Fund, unaotumia fungu lake, kukabili maradhi ya Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu duniani, mwaka huu ikiwa na bajeti ya Dola Bilioni 5 (sawa na Sh. trilioni 13,445).

Hao waraibu nchini, wana maoni kwamba mfuko huo uwatambue rasmi kama kundi maalum linalostahili ufadhili wa huduma za afya.

Mtazamo uliopo katika ombi hilo ni kwamba upatikanaji wa fungu hilo utasaidia kupunguza maambukizi hayo na kuboresha maisha yao pamoja.

Ndani ya utekelezaji wake, inaangaliwa kuwapo sera za kitaifa za kupunguza madhara kwa watumiaji dawa za kulevya nchini.

Kihistoria, mtazamo na uwapo wa Global Fund ya sasa, unaanzia namna ya kutafuta majibu kuanzia mwaka 2000, dhidi ya athari za maradhi tajwa; Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu, ikifanyiwa mapitio mathalan kwa wachangiaji mataifa tajiri duniani, maarufu G8.

Kutimu mwaka 2001, mtazamo ukafika katika vikao vya Umoja wa Afrika (AU), kabla ya kupewa baraka na Umoja wa Mataifa mwaka huo, kisha kurejea mikononi mwa G8, iliyotimiza baraka zake Global Fund ikaanza kutumika mwaka unaofuata 2002.

UMUHIMU NCHINI

Ndani ya mtazamo huo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Watu wanaotumia Dawa za Kulevya nchini Tanzania (TaNPUD), Juma Kwame, anaeleza umuhimu wa kuwa na sera za kupunguza madhara kwa watumiaji dawa hizo.

Kupitia kikao kilichofanyika makao makuu ya ofisi hizo, kuna asasi za kiraia zaidi ya 10 zinazofanya kazi ya kupunguza madhara kwa watumiaji dawa za kulevya nchini, zilijadili changamoto zinazowakabili waraibu wanaopata huduma za upunguzaji madhara

Ni kikao kilichoambatana na kingine kama hicho cha majadiliano, kati ya TANPUD, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kuleya (DCEA) na CDC, kupitia mradi unaoitwa ‘Compass’.

Hiyo inalenga kuchechemua (advocacy) na kupanua wigo wa huduma za upunguzaji madhara kwa asilimia 20 katika maeneo yenye uhitaji na huduma za afya ya akili.

“Kupitia lengo hilo, waraibu wanaotumia dawa za kulevya watapata huduma za kinga, upimaji na matibabu ya Ukimwi katika ‘Mat clinic’ (vituo tiba saidizi kwa waraibu wa dawa za kulevya) na mradi wa mabomba ya sindano kwa wanaojidunga mradi huu unasimamia…” anatamka Kwame.

Mdau huyo anaeleza kuwapo sera ya upunguzaji madhara kutasaidia kutoa mwongozo na kuongeza ufanisi wa kuhudumua waraibu wa dawa za kulevya nchini, huku akitaja ukosekanaji wa sera inazaa changamoto kubwa kukabili madhara hayo.

Aidha, Kwame anaeleza tatizo la utumiaji dawa kupitiliza kwa waraibu wake, inawahatarisha wahusika kupoteza maisha.

Inatajwa kwamba kukosekana dawa tiba anayoitaja kwa jina ‘Naloxone’ katika vituo vya afya jirani, hata ngazi ya jamii, imekuwa changamoto kubwa.

 

“Watumiaji wa dawa aina ya ‘heroin’ ndio hupata changamoto ya ‘overdose’ (ziada ya matumizi), serikali imejitahidi kuhakikisha zinapatikana katika vituo vya kutoa huduma (MAT clinic).

“Kuna wakati waraibu wanalalamika, upatikanaji wa huduma hii baada ya saa za kazi kwisha katika kliniki za MAT,” anasema Kwame’

Anasema serikali na wadau wanatafuta njia sahihi za kupunguza madhara kwa watumiaji, ikiwamo huduma za ‘methadone’ kwa waraibu.

“Tumeona udhibiti umekuwa mkubwa, katika hili tunaipongeza mamlaka (DCEA), hata upatikanaji dawa aina ya ‘heroin’ umekuwa mdogo na hiyo inayopatikana, imechakachuliwa. Watumiaji huchanganya na kemikali mbalimbali ili kuongeza makali,” anasema Kwame.

Kimsingi, heroin imo katika dawa za kulevya zinazoongoza kwa ukali na madhara yake.   

SHIDA YA MAGONJWA

Kwame anaeleza, watumiaji dawa za kulevya wanakabiliwa na magonjwa ya kuambukiza ikiwamo Ukimwi, Homa ya Ini na Kifua kikuu.

Ni kikao kilichohudhuriwa na wadau kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), pia NASHCOP, ambayo ni Programu ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukimwi na magonjwa ya zinaa (STI), hali kadhalika asasi ya CDC.

Mwakilishi kutoka TACAIDS, Dk. Neema Shikiwe, anasema Mkakati wa Tano wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/26, unalenga kuimarisha usawa na kuvunja makundi kwa yale yaliyoachwa nyuma.

Anataja kipaumbele ni kuzingatia kinga za msingi dhidi ya VVU kwa wanaojidunga, kuna hatari ya maambukizi kupitia kujidunga sindano.

 

“Ni muhimu kwa wanaojidunga kupima maambukizi ya Ukimwi na Homa ya Ini, pamoja na kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kutumia dawa kinga au kondomu,” anasema.

Pia, Dk. Neema anawaasa kuendelea kuelimisha na kuanzisha kampeni za kupunguza madhara kwa watumiaji dawa za kulevya.

“PREP ni dawa kinga ambazo mtu anatumia kujikinga ili asipate maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kama ilivyo ‘p2’ kama njia ya kuzuia mimba,” anafafanua Dk. Neema.

Mratibu wa NASHCOP, Dk. Barnaba Gabriel, anasema serikali kupitia Wizara ya Afya, imeweka mpango mkakati wa kuanza kuhudumia Homa ya Ini ‘B’ na ‘C’ kwa makundi maalum, ikipunguza madhara, ikiwamo kwa wanaojidunga dawa za kulevya.

Anataja maambukizi ya Homa ya Ini ‘C’ nchini ni asilimia 0.2, lakini kwa wanaojidunga sindano wanaonekana kwa asilimia 50 hadi 70.

Dk. Barnaba anaeleza Homa ya Ini ‘B’ huambukizwa kupitia ngono bila kinga, mama kwenda kwa mtoto lakini Homa ya Ini ‘C’ inaambukizwa kwa njia ya damu, ikiwamo kuchangia sindano wakati wa kujidunga.

“Dalili kuu mbili za kubaini kuwa umepata maambukizi ya Homa ya Ini ‘C ‘ni kukojoa mkojo mweusi, pamoja na kupata rangi ya manjano kwenye ngozi na machoni.

“Kama tunavyofahamu dalili hizi huonekana katika hatua za mwisho za ugonjwa, pia kupungua uzito, kuumwa kichwa sana na mwili kuchoka,” anasema Dk. Barnaba.

Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2023 nchini, inaeleza mpango mkakati wa kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, ikilenga kutoa tiba, utengamano na ushauri kwa waraibu, ikizingatiwa Sera ya Taifa ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024, ikitaka upunguzaji madhara kwa waraibu.

Ripoti inainisha maeneo ya msingi ya utekelezaji wa mkakati, ni kuratibu matibabu ya waraibu, kuandaa miongozo tiba, pamoja na usimamizi shirikishi katika vituo vinavyotoa huduma hizo kwa waraibu.

Inaelekeza wenye uraibu kupatiwa tiba katika vituo kwenye vitengo vya afya ya akili waliokuwapo, 903,062; wanawake 32,738 na wanaume 470,324.

RIPOTI DAWA KULEVYA 

Ripoti ya DCEA ya mwaka 2018, inaonyesha kuwa takriban nusu ya vifo vinavyohusiana na matumizi ya dawa za kulevya, vilisababishwa na Homa ya Ini aina ‘C’; ikionyesha ni sehemu ya madhara makubwa ya 

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wa mamlaka hiyo anasema: “Naloxone inapatikana katika vituo vya kutolea huduma vya serikali, hata hivyo anawataka watakaopata tatizo la uzidishaji wa dawa wapige namba 119 ili waweze kusaidika popote walipo”.