Viongozi wa dini wasisitiza amani kuelekea uchaguzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:51 PM Apr 25 2025
Mchungaji Patrick Muthee kutoka nchini Kenya akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwaajili ya kushiriki Wiki ya Uamsho na Kuliombea Taifa
Picha: Mpigapicha Wetu
Mchungaji Patrick Muthee kutoka nchini Kenya akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwaajili ya kushiriki Wiki ya Uamsho na Kuliombea Taifa

Watanzania na wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wametakiwa kuendeleza na kudumisha amani, hasa katika kipindi hiki ambapo Tanzania inakaribia kufanya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mchungaji Patrick Muthee kutoka Kenya, ambaye ni miongoni mwa viongozi wa dini walioko nchini kwa mwaliko wa Kwaya ya Gethsemane Group Kinondoni (GGK) ya Kanisa la Waadventista Wasabato, Kinondoni, Dar es Salaam. Viongozi hao wa dini wamealikwa kushiriki Wiki ya Maombi Maalumu kwa ajili ya kuiombea Tanzania amani, mshikamano na upendo.

“Tumekuja kuungana na ndugu zetu wa GGK kwa ajili ya maombi. Kwa kuwa Tanzania inaelekea katika Uchaguzi Mkuu, tumeweka kipaumbele katika kuiombea nchi hii amani, umoja na mshikamano. Tunaamini kwa maombi, Taifa litaendelea kuwa na utulivu,” alisema Mchungaji Muthee.

Ameongeza kuwa Kenya na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu enzi za harakati za kupigania uhuru, na kwamba uhusiano huo umesaidia makanisa ya nchi hizo kushirikiana kwa karibu katika kuhubiri Injili.

Kwa upande wake, Mchungaji Harun Muturi Mwangi kutoka Nairobi, Kenya alisema lengo la kushiriki wiki hiyo ni kuamsha ari ya kiroho kwa waumini wa Tanzania na Kenya pamoja na kuiombea dunia kwa ujumla.

“Tumekuja kwa mwaliko wa Kanisa la Kinondoni kwa ajili ya wiki ya uamsho. Tutaungana na Watanzania katika maombi kwa ajili ya uchaguzi wa Tanzania ili amani iweze kutawala. Tunawaombea Watanzania waendelee kuwa watu wa amani kama walivyo sasa,” alisema Mchungaji Harun.

Mwenyekiti wa Kwaya ya GGK, Samora Sadick, alisema wiki ya maombi inaambatana na nyimbo za Injili zenye ujumbe wa kuhamasisha upendo, mshikamano na amani nchini.

“Tumeandaa kipindi hiki kwa ajili ya kuimba pamoja, kufahamiana na kujiandaa kiroho ili sote tuwe tayari kulithi makao ya mbinguni. Tunawaalika Watanzania wote kushiriki nasi,” alisema Sadick.

Maombi hayo yatadumu kwa wiki moja kuanzia Aprili 27 hadi Mei 3, 2025, kuanzia saa 10 jioni kila siku. Wahubiri mbalimbali kutoka Kenya na Tanzania watashiriki kuongoza mahubiri na maombi hayo.

Akizungumza wakati wa kuwapokea wageni hao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mchungaji Victor Chihimba wa Kanisa la Waadventista Wasabato Kinondoni alisema:

“Kama Kanisa, tunatambua umuhimu wa kuliweka Taifa mikononi mwa Mungu, hususan katika kipindi hiki nyeti. Hivyo wiki hii itakuwa ni ya baraka, maombi na kuombea amani, upendo na mshikamano kwa nchi yetu.”

Mchungaji Chihimba pia ametoa wito kwa Watanzania wa dini zote kushiriki katika juma hilo la kipekee, akisema kuwa tukio hilo limekuwa likifanyika kila mwaka na limekuwa chachu ya kuwaleta watu pamoja kiimani na kijamii.