Wajitokeza kuchukua fomu kuwania ubunge

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:16 PM Jul 02 2025
Wajitokeza kuchukua fomu kuwania ubunge
Picha: Nipashe Digital
Wajitokeza kuchukua fomu kuwania ubunge

WAKATI mchakato wa uchukuaji fomu za kuwania nafasi ya ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukiendelea waliokuwa wabunge na ambao wanawania kwa mara ya kwanza, wamejitokeza maeneo tofauti nchi kuchukua fomu.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ushetu, lililopo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani, leo Julai 2, 2025, amechukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Fomu hiyo ameirejesha katika Ofisi za CCM Wilaya ya Kahama na kukabidhi kwa Katibu wa chama hicho, Endrew Chatwanga.

Cherehani aliingia madarakani mwaka 2021 kupitia uchaguzi mdogo uliofanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hayati Elias Kwandikwa.

Pia, mjasiriamali wa kata ya Chiwale halmashauri ya wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, Mwanaisha Liyhuka amechukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Ndanda, kisha kuirejesha rasmi.

Kadhalika mwalimu wa shule ya msingi Chakama, iliyopo halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara, Furaha Namele, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Masasi Mjini na tayari mwalimu huyo amerejesha fomu katika ofisi za CCM Wilaya ya Masasi.

Wakili Chrispine Simon, amechukua na kurudisha kuomba ridhaa ya kuteuliwa na CCM, kugombea ubunge katika Jimbo la Itwangi.

Amechukua fomu hiyo leo Julai 2, 2025 katika Ofisi za CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Akizungumza mara baada ya kuchukua Fomu hiyo, amesema yeye kama Kijana mzalendo,ameamua kutumia haki yake ya kikatiba kuchukua Fomu ya Ubunge,na kwamba anasubili taratibu zingine za kichama.

Naye Wakili Danford Mpelumbe amechukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Masasi Mjini na kuirejesha rasmi leo.

Huko Chunya, mfanyabiashara wa madini katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Geofrey Mwankenja amechukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya CCM, kumteua kukiwakilisha kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Lupa, wilayani humo.

Mwankenja amechukua fomu hiyo ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kuwania nafasi hiyo, alianza kwenye uchaguzi Mmkuu wa mwaka 2015, akashindwa na baadaye akaomba 2020 pia alishindwa.

Amesema ameamua kuomba nafasi hiyo, ili kutimiza haki yake ya kikatiba na kwamba endapo chama hicho kitampa nafasi hiyo na akashinda, atahakikisha anaisaidia serikali kuwahudumia wananchi kwa kutumia raslimali zake binafsi.

Miaka mitano iliyopita, Jimbo la Lupa lilikuwa linaloongozwa na Masache Kasaka (CCM) ambaye pia amechukua fomu ya kutetea jimbo hilo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Pia, aliyekuwa Mbunge wa CHADEMA, Asia Mwadini Mohamed atimkia CCM kugombea ubunge Jimbo la Kijini Kaskazini Unguja. 

Imeandikwa na Rahma Suleiman, Shaban Njia, Nebart Msokwa, Hamisi Nasri, Marco Maduhu na Boniface Gedion