Wananchi Kibaha wapatiwa hatimiliki za ardhi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:04 PM Sep 03 2025
news
Picha Julieth Mkireri
Mkuu wa Wilaya.ya Kibaha Wilaya Nickson John akiwa anaonyesha ramani kwa wananchi wa Pangani

MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ameanza kugawa hatimiliki kwa wakazi wa mitaa mitatu iliyopo kata ya Pangani wilayani humo, na kwamba hatua hiyo linaenda kuondoa migogoro ya ardhi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo katika mtaa wa Kidimu, John amesema katika awamu ya kwanza hati zaidi ya 180 zimegawiwa kati ya hati 7000 ambazo zipo tayari.

Mkuu huyo wa wilaya amesema hadi sasa ni viwanja 18,000 vimepimwa na kwamba utoaji wa hati unaendelea kulingana na namna wananchi wanavyoendelea kulipia.

"Leo tunaanza kutoa hati 180 kwa atakayekamilisha malipo atapata hati yake na ramani 5000 tayari zipo tayari ambazo wananchi watapata bure," amesema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dk. Rogers Shemwelekwa amewatahadharisha wananchi waliopata hatimiliki na ambao wapo kwenye mchakato kuepuka kuuza maeneo yao.

Wananchi wa kata ya Pangani walioshiriki hafla ya utoaji wa hatimiliki
"Msiuze viwanja ambavyo tayari vimesajiliwa msivigawe na kuviuza fuateni taratibu na msikubali kupotoshwa," amesisitiza.

Amesema lengo la mradi huo ni kuwasaidia wananchi kupimiwa maeneo yao na kupata hatimiliki ili waweze kuepuka migogoro.

Msajili wa Hati Msaidizi wa mkoa wa Pwani Burton Rutta amewasisitiza wakazi wa Kata ya Pangani kuhakikisha wanapata hatimiliki ya maeneo yao ambazo zitawasaidia kutumia kwenye mambo mbalinbali muhimu.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Pangani Clementina Mwankenja ameishukuru serikali kwa kufanikisha utoaji wa hati hizo huku akiomba kuboreshewa miundombinu ya maji na umeme.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa.