AIDA KENANI WA NKASI KASKAZINI; Kaanza safari viti maalum ana Sh. 1000

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 12:45 PM Apr 02 2025
Mbunge Aida Kenan, akihojiwa na mwandishi wa habari
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge Aida Kenan, akihojiwa na mwandishi wa habari

JIMBO la Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa limefanya mabadiliko makubwa, kwa uamuzi wa kumchagua mbunge pekee mwanamke kutoka chama cha upinzani na kuleta mageuzi ya kidemokrasia kwenye jimbo hilo.

Aida Kenani, alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ilikuwa simulizi ya vishindo kumwangusha aliyekuwa mbunge anayeshikilia jimbo hilo kwa miaka mingi kutoka chama tawala (CCM), Ally Kessy.

Kisiasa ikamkweza sana Aida, hata akapata umaarufu kupitia mambo matatu, kwanza kumshinda mpinzani wake aliyekuwa machachari katika kipindi chake cha ubunge; pili kuwashinda vigogo wa chama chake CHADEMA katika mchakato kura za maoni. 

Vilvile kuna umachachari wake, kwamba akagomea msimamo wa chama uliowataka wabunge asiende bungeni, kwa madai hakikuutambua uchaguzi huo.

“Namshukuru Mungu hata kufika leo, nilianza safari ya kisiasa katika mazingira tofauti, kwa nafasi ya chini ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huko Sumbawanga mkoani Rukwa.”

Anasema yeye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA), mkoa wa Rukwa na aliwahi kuwa Katibu Mwenezi na baraza hilo mkoa, kuanzia mwaka 2014 hadi mpaka 2019.

“Sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote zaidi ya CHADEMA, lakini baba yangu mzazi Joseph Kenan, alikuwa kiongozi wa CCM, hata wakati napata ubunge alikuwa huko kwa hiyo vita yake ilikuwa sio ndogo,” anasema.

Aida anasema, kadri anavyoendelea kupambania ndoto yake akiwa kwenye chama chake, wazazi na ndugu zake walianza kumuelewa.

Wakati anaanza ilikuwa jambo gumu watu kumkubali na kumsikiliza, kwa sababu yeye ni mwanamke.

APAMBANA NA WENYE ELIMU

“Wengi walikuwa na Masters (shahada ya pili) wengine PhD, peke yangu

ndio nilikuwa na Diploma wakati huo ya Maendeleo ya Jamii. Lakini cha kushangaza, niligombea nafasi ya

BAWACHA na BAVICHA na nilishinda kote na wakati huohuo ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na Nilipewa nafasi zote hizo wakiwa wananijaribu.

Lakini, kadri walivyoona nafanya vizuri ndio wakawa wananiamini na kunipatia nafasi nyingine hizo zilizofuata, akifafanua wakati huo anaaminiwa katika nafasi hizo, alikuwa na umri mdogo sana.

“BAWACHA nilikuwa naongoza wanawake ambao wamenizidi umri na baada ya kuona nimeweza kuongoza katika nafasi hizo zote, mwaka 2015 nikawaambia kumbe naweza kugombea udiwani.

“Wakaniambia gombea ubunge...nikawaambia hapana, huko ni mbali sana sitaweza, lakini walinisisitiza kwamba naweza!”

ASAKA UBUNGE NA SH. 1000

Aida anasimulia, siku alienda uchaguzi wa kura ya maoni ya kutafuta ubunge wa viti maalum ndani ya chama chake, alikuwa na Sh.1000 mfukoni, nauli ya kumpeleka eneo la tukio na kumrejesha nyumbani kwake.

Mbali na siasa, anasema alikuwa anafanya shughuli ndogo za ujasiriamali, ikiwamo kutengeneza sabuni, mishumaa na mafuta zilizompatia kipato.

“Hata siku yenyewe niliyokwenda wala sikuwa ‘serious’ (makini), yaani niliona tu kwamba ngoja niende nikashiriki

nione inakuwaje, lakini jambo la kushangaza, nilikuwa mshindi wa kwanza.

“Katika wapiga kura 93, nilipata kura 81, wengine waliambulia kura moja wengine, sifuri” anasimulia.

Anasema, alivyoshinda kura za maoni kwa wanawake, akaenda kujaribu tena kwa ngazi ya vijana, akiwa na simulizi:

“Huko nako nikashinda kimkoa na kanda. Kwa hiyo, nilishinda kura za maoni sehemu tatu, kupitia vijana, wanawake na udiwani viti maalum.

“Na nilifanya hivyo, nikiwa najaribu kote ili kokote bahati itakakoangukia ndio huko huko, isipokuwa iwe ndani ya CHADEMA,” anasema Aida.

“Vikwazo vilianza, wengine walisema nina umri mdogo na wakati huo nilikuwa na miaka 24, hivyo siwezi kuwakilisha vizuri bungeni, wengine wakasema familia yangu ni CCM kwa hiyo hawaniamini, yaani kuliibuka

vikwazo vingi.

UBUNGE VITI MAALUM

Katika utaratibu wa chama chake, anasema huwa wanapatiwa maeneo kadhaa ya kuyawakilisha. kuna mwaka wanapunguziwa, ili katika hayo majimbo aliyopewa aanze kutafuta jimbo la kugombea. 

“Kwa hiyo nilijiapiza kwamba, nitakuwa mbunge wa viti maalumu awamu moja na kilichonifanya nijiwekee huo utaratibu. 

“Niligundua kwamba kila nikisimama kuzungumza jambo bungeni labda la wananchi walilonituma au kuuliza swali au kuchangia,yaani mbunge wa jimbo husika anaona kama sistahili kufanya hivyo bali yeye mwenye jimbo lake,” anaeleza.

Anasema, katiba ya nchi inamtambua mbunge wa kuteuliwa wa viti maalum au wa kuchaguliwa jimboni, akisema wote wana haki sawa, lakini yeye kutokana na mazingira aliyoyaona hakutamani kuendelea kwa kipindi kingine kuwa mbunge wa viti maalum.

ALIVYOJITOSA NKASI KASKAZINI

Baada ya kuamua kwenda Jimbo la Nkasi Kaskazini, anataja haikuwa kazi rahisi kwake, kwa sababu kulikuwapo mbunge wa CCM wakati huo, Ally Kessy, ambaye baada ya kugundua kwamba ana mpango wa kugombea huko, naye akaanza kupambana naye.

Aida anataja mbinu ya upande wake akawa anawaelimisha wananchi wake kwamba “kiongozi sio lazima awe na fedha, bali mwenye uwezo wa kuwatumikia wananchi wake kwa dhati...”

ATWAA JIMBO

Anasimulia, namna siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Mwaka 2020, mpinzani wake alikuwa na furaha kubwa kabla ya kutangazwa matokeo akiamini atashinda, lakini hakuamini kilichotokea baada ya matokeo kutangazwa.

Anasema wakati yeye anasubiri nakala halisi za matokeo ziletwe katika maeneo yaliyokuwa yamebaki, mpinzani wake na wafuasi wake walikuwa wameanza kushangilia, wakidai wamepata matokeo ya maeneo yote, hivyo wameshinda.

“Sasa nikawa nashangaa ameshindaje wakati bado nakala nyingine hazijaletwa na wakati huo matokeo mengine yaliyokuwa yameletwa mimi nilikuwa nayo mkononi na yakinionyesha kwamba alikuwa bado hajashinda?

“Kwa hiyo wakatupa saa moja kila mgombea akusanye matokeo kutoka kwenye kata ambazo zilikuwa hazijaleta matokeo na ambazo ziko zaidi ya kilomita 90. 

“Nilifanya kila ninavyoweza, nikatafuta pikipiki na kabla ya muda tuliyokuwa tumepewa tukawa tumepata yote. Sasa wakati yamejumuishwa nikaona ghafla zile shangwe ambazo mpinzani wangu alikuwa ameanza zinatulia,” anasema.

Mbunge huyo anaeleza kwamba, baada ya matokeo yote kuletwa kwao, kura zilihesabiwa upya na yeye akaongoza na baada ya mpinzani wake kubaini ameshindwa uchaguzi, aliamua kuondoka kwa hasira.

“Baada ya kutangazwa, nilishusha pumzi, maana mapambano yalikuwa ni makali kupitiliza. 

“Baadaye kidogo ndio nikawasha simu zangu kufahamu kinachoendelea kwa wagombea wengine wa chama changu na nikaishia kupata taarifa za kusikitisha kwamba wenzangu karibu wote hawakutangazwa.

“Badala ya kushangilia ushindi, kwangu ilikuwa huzuni, maana sikuamini kilichotokea kwenye uchaguzi ule kwa wenzangu. 

“Nilikosa nguvu kabisa na wakati huo wapiga kura wangu wenyewe walikuwa na furaha kupitiliza na wakawa wanaendelea na shamrashamra,” anaeleza.

UAMUZI MGUMU

Licha ya chama chake kutangaza kutoutambua uchaguzi huo wa mwaka 2020. Aida anasema, alichukua uamuzi mgumu kwenda bungeni baada ya shinikizo kutoka kwa wapigakura wake.

“Nilitafakari sana kwamba sasa nafanyaje katika ‘situation’ (hali) kama hii, watu wengi walinishauri kutoka maeneo tofauti na wakati huo chama changu kikawa kimetoa msimamo kuhusu uchaguzi huo. 

“Kwa kweli nilikuwa njiapanda kwa sababu licha ya msimamo wa chama. Lakini wapigakura hawakuelewa, wakasema kwamba ni lazima niende bungeni nikawawakilishe.

“Kwa sababu mimi ndiye mbunge wanayemtaka kwa wakati ule.Endapo sitakwenda hawako tayari kunipigia kura tena wakati mwingine,” anasimulia msukosuko huo ulivyokuwa jimboni kwake.

Pia, anasema ushindi wake ulisaidia kuondoa omani iliyokuwapo awali kwamba ni “wenye fedha pekee ndio

wanashinda au ndio wanafaa kuwa viongozi,” kwa sababu

hata yeye ametoka kwenye familia ya kawaida.

AVUTIA WASICHANA

Kwa sasa jimboni kwake, wasichana wengi wanatamani kuwa kama yeye na mara nyingi wanamfuata kumwomba ushauri, namna ya kuingia kwenye sekta hiyo.

Anasema katika miaka ya nyuma, idadi ya wanawake waliokuwa wakisimama kugombea nafasi mbalimbali, ilikuwa ndogo sana na wakati mwingine kukosa kabisa, lakini katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, asilimia 80 ya wanawake waligombea katika uchaguzi huo.

MFUKO WA JIMBO

Aida anasema wananchi wanasema kabla ya yeye kuwa mbunge katika jimbo hilo, walikuwa hawajui kama kuna mfuko wa jimbo, lakini kupitia yeye wamefahamu.

“Walikuwa hawafahamu kama kuna kitu kinaitwa mfuko wa jimbo. Sasa nilivyokuja mimi, nikawaambia na nikawauliza wanataka fedha hizo za mfuko zitumike kwenye miradi gani?

“Kwa hiyo wao ndio huwa wanapanga kwa kunishirikisha, wanaangalia kwanza jambo gani la muhimu halafu ndilo tunaanza nalo, tunaenda hivo hivo kwa awamu kulingana na umuhimu jambo,” anaeleza 

WANAVYOMZUNGUMZIA AIDA

Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Sharifa Suleiman, anasema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika jamii kupitia uwakilishi wao katika vyombo mbalimbali, vikiwamo vyombo vya uamuzi kama bunge na serikali.

Mwenyekiti wa ChademaTaifa, Tundu Lissu, anasema katika uongozi wa Aida ndani ya chama hicho, amefanya kazi nzuri hasa kuwainua wanawake na wasichana kuingia kwenye siasa.

Lissu anasema, kutokana na mchango wake Machi 8 mwaka huu, katika sherehe zilizoandaliwa na wanawake wa chama hicho kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, wenzake hao walimpatia tuzo kutokana na mchango wake huo.

WAPIGAKURA WAKE

Joshua Noel, ni mfanyabiashara wa mji wa Namanyere mkoani Rukwa, anayesema licha ya kuwa mbunge pekee mwanamke kimkoa, uwapo wake umesaidia kuamsha ari ya kisiasa katika eneo lao, hasa wanawake na mabinti.

Kadhalika, anasema kazi zake alizofanya kwa miaka mitano hususan kupitia mfuko wa jimbo zimeonekana wazi.

Leticia Charles, mpiga kura kutoka Kata ya Kilando, anasema mfuko wa jimbo

 kupitia Aida, umesaidia hata wanawake kuaminiwa na kuruhisiwa na waume zao kuingia kwenye siasa.

“Sasa hivi tumepata nguvu ya kuomba ruhusa kwa waume zetu kwenda kugombea, mfano mwaka jana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, wanawake wengi walijitokeza.

“Aida ametuonyesha njia, zamani huku watu walikuwa wanaona siasa ni kazi ya wanaume tu, lakini sasa hivi hiyo haipo, wote tunapambana na tunashindana kwenye sanduku la kura,” anasema Leticia.