ZAMA hizi kujifunza lugha za kigeni ni jambo muhimu kwa sababu hupanua mtazamo wa masuala mbalimbali na uelewa kuhusu dunia.
Lugha ni ujuzi unaoboresha uwezo wa kuwasiliana na watu wa mataifa mbalimbali, kuongeza ujuzi wa utambuzi, pia kufungua milango kwa fursa za kazi na uzoefu wa kiutamaduni.
Ndiyo maana ukiwa na utajiri wa lugha una nafasi ya kujikwamua na shida ya kokosa kazi au ajira kwa sababu unaweza kuwa mkalimani, mwongoza watalii, mwalimu na hata mfanyakazi kwenye kampuni au viwanda vya kutoa huduma za lugha ya kigeni unayoifahamu.
Naibu Mkurugenzi wa Kituo Cha Utamaduni wa Ujerumani Tanzania Goethe Institut na Mkurugenzi wa Lugha wa Taasisi hiyo, Nassoro Nascov, anazungumza na Nipashe, kuhusu nafasi ya Kijerumani katika kuwasaidia Watanzania.
Anasema kuwa unaposoma lugha za kigeni hasa Kijerumani anajiweka pazuri kwenye soko la ajira kwa sababu asilimia kubwa ya wengi waliosoma lugha hiyo wameajiriwa, kwa lugha hiyo kutumika katika mataifa mbalimbali duniani.
Goethe Institut, inayofundisha na kusambaza lugha hiyo inasisitiza kuwa unaposoma Kijerumani unajiweka katika soko la ajira.
Nascov anaongeza kuwa pamoja na majukumu mengine ya ushirikiano katika utamaduni pia taasisi hiyo inatoa ufadhili katika masuala mbalimbali ya utamaduni, wasanii kuimba, kuchora, ngoma za utamaduni na kushirikiana na balozi za nchi mbalimbali kwa kufanya makongano ya pamoja.
Nascov anazitaja faida kadhaa ambazo mtu anaweza akazipata akijifunza lugha hiyo kuwa ni elimu na ujuzi wenye asili ya taifa hilo.
"Lugha ni sehemu utamaduni kwa mfano Mzaramo anazungumza Kizaramo kitu cha kwanza kinacho mtambulisha mtu ni lugha yake. Sasa tukirudi kwenye Kijerumani, Ujerumani ni taifa lenye uvumbuzi wa aina mbalimbali kuanzia sayansi, teknolojia kwa hiyo kukisoma hakumfanyi mtu ajue kukiongea pekee hapana, atakutana na fursa nyingi kwa kuwa ni lugha muhimu kwa wataalamu wa utafiti katika mambo mbalimbali ya kitaaluma.”
Anaongeza:"Faida za kukijua Kijerumani kwa Ujerumani ngazi ya chuo kikuu kama mtu atakuwa amesoma kufikia daraja la juu kwa vyuo vya serikali anasoma bure hii ni fursa kwa Watanzania.” Anaeleza.
Anaendelea na ufafanuzi kwamba kwa mtu mwenye elimu ngazi ya stashahada Ujerumani ina utaratibu wa kuwapatia fursa mbili kujifunza bure na kufanya kazi nusu ya muda wa kazi , mathalani ikiwa ni saa 12 atafanya saa sita na atalipwa.
Nascov anasema vitu hivyo vinakwenda sambamba na pia anapewa fedha mwisho wa mwezi, akisema anaona ni mfumo mzuri kwa vijana wa Tanzania ambao kwa kujua Kijerumani wanaweza kupata fursa nyingi.
Mkurugenzi huyo wa lugha, anasema mbali na elimu kwa sasa Ujerumani ni nchi inayohitaji nguvu kazi kuna watu ambao wameshahitimu wanaweza kupata fursa ya kwenda kufanya kazi kihalali kwa sababu wanajua lugha hiyo.
Mpaka sasa katika chuo chao kilichopo Upanga Dar es Salaam wako wanafunzi wengi waliowafundisha kutoka ndani na nje kama Cameroon, Malawi, DRC, Zambia na Burundi.
Anapoulizwa ni namna gani lugha hiyo inafundishwa anasema ni kwa kufuata mfumo wa ufundishwaji lugha wa Ulaya na kuna hatua sita ambazo mwanafunzi anapitia ambazo ni A1 A2 B1 B2 C1 C2.
Anafafanua kuwa hatua hizo zinategemeana na uhitaji wa mtu anavyoweza kujifunza na inaweza kumchukua miezi tisa hadi 12 kujua Kijerumani.
OMBI KWA TANZANIA
Nascov anaiomba serikali iingize Kijerumani kwenye mtaala wa sekondari kwa sababu taasisi yao haiwezi kuwafikia watu wanaopenda kukisoma japo wahitaji ni wengi.
Anasema serikali ikiingiza lugha hiyo wataanza kuandaliwa kuanzia sekondari na watakapohitimu watakuwa na ujuzi wa lugha.
Anaongeza kuwa mwaka 2009 walishirikiana na serikali katika kufanya majaribio ya kufundisha lugha hiyo katika shule za sekondari za Zanaki na Chang’ombe na kwamba tangu wakati huo wanafunzi wengi walijifunza Kijerumani na hao wanaosoma somo hilo pia wanafanya vizuri katika masomo mengine tofauti.
Aidha, anasema sehemu ya kwanza ya wanafunzi waliomaliza katika shule hizo wako masomoni nchini Ujerumani wanasoma ‘masters’ wengine wameajiriwa sehemu mbalimbali ikiwamo ubalozini na wengine ni walimu.
“Shuleni kwetu tunapokea wanafunzi 200 kwa kila msimu wa masomo na ada yake ni kuanzia Sh. 750,000 hadi 1,100,000 kwa sasa tumepunguza ada ili watu waweze kumudu kufikia hatua ya B1 B2 ambayo inamwezesha mtu kupata sifa akiwa na taaluma aliyesomea kuajiriwa Ujerumani moja kwa moja,” anasema.
Aidha, anasema tayari kwa mwaka huu si chini ya wanafunzi 600 wamepita katika mikono yao na walimu walionao shuleni ni Watanzania hatua ya kutumia walimu wazawa akiamini imepunguza tatizo la ajira nchini.
Anasisitiza wanafunzi wengi wakijifunza lugha hiyo itapunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa sababu ina fursa akisema inazungumzwa na watu milioni 130 dunia na sio tu Ujerumani.
“Kuna nchi tano zinazotumia lugha hiyo kama Luxenborg, Austria, Ubelgiji, Uholanzi na Uswizi.”
Anasema pia wana mawasiliano na kampuni kubwa za utalii ambayo huomba wafanyakazi wake wafanyiwe mafunzo ili waweze huzungumza na watalii kutoka Ujerumnai wanpokuja nchini na kwamba kwa kufanya hivyo huongeza wigo wa kutembelea hifadhi za taifa.
“Watalii wengi wa Ujerumani wanapenda kuongozwa na anayejua lugha yao kwa sababu ndio njia pekee ya kuwavuta zaidi kuja nchini kwetu kutalii,” anasema Nascov.
Kadhalika, anasema wana ushirikiano na wa karibu na Wizara za Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Elimu, Sayansi na Teknolojia na kwamba wiki mbili zilizopita walikwenda Zanzibar kwa mazungumzo na serikali imekubali wazo la Kijerumani kuingizwa katika mitaala ya elimu.
Pia, anasema walikutana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kujadili namna gani Kijerumani kinaweza kuingia katika mitaala ya elimu nchini.
Hata hivyo, anasema mawazo ya wizara isiwe lugha ya kujifunza kuanzia sekondari pekee bali wanapenda iwe kuanzia shule za msingi japo kwa sasa makubaliano yaliyopo waanzie sekondari baada ya hapo wataangalia namna ya kuanzia ngazi za chini.
“Baada ya kupata mafunzo hayo muhitimu anaweza kupeleka maombi ya kazi Ujerumani lakini uzuri uliopo kuna taasisi itaanza kazi karibuni ikiwa mahusi kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kwenda nchini huko kwa masuala mbalimbali kama kubadilishana utamaduni na kuongeza ujuzi katika mambo mbalimbali.
SAUTI YA MNUFAIKA
Julius Kileo, ni mmoja kati ya wanufaika wengi waliojifunza Kijerumani kupitia taasisi ya Goethe katika Sekondari ya Chang’ombe anayesema amefaidi kutokana na kujifunza lugha hiyo.
Anaongeza kuwa kwa sasa ni mwalimu anafundisha lugha hiyo na ni jambo lililobadili miasha yake kiujumla.
Halikadhalika Kileo anasema mwanzoni wakati anajifunza lugha hiyo hakuamini kama siku moja inaweza kubadili maisha yake bali alijifunza kwa kuwa alipenda kukijua Kijerumani na sasa anashangilia mafanikio makubwa aliyoyapata.
“Ninashauri serikali iweke nafasi ya kutosha wanafunzi kujifunza lugha za kigeni ili kufungua milango ya biashara na ajira niwatake wanafunzi walio hitimu vyuo mbalimbali wajifunze Kijerumani watapata fursa nyingi.”
“Serikali ishirikiane na Taasisi ya Goethe kuipa nguvu, watu wengi watambue kama wanatoa mafunzo hayo kwakuwa watakaojua lugha hiyo watakuwa katika nafasi ya kuajiriwa na kupunguza tatizo la ajira nchini” anasema Kileo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED