Mdereva 400 Ilala wapatiwa elimu kupunguza ajali

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 04:39 PM Jul 02 2025
Mdereva 400 Ilala wapatiwa elimu kupunguza ajali
Picha:Mpigapicha Wetu
Mdereva 400 Ilala wapatiwa elimu kupunguza ajali

KATIKA kupambana na ajali za barabarani zinazo sababishwa na baadhi ya madereva kutokuwa na elimu ya usalama barabarani, Wilaya ya Ilala imeamua kuwakutanisha pamoja madereva wa bajaji, guta za umeme na bodaboda kuwapatia elimu ili kupunguza ajali hizo.

Mafunzo hayo yaliyotumia muda wa wiki mbili yaliendeshwa na Jeshi la Polisi, na kisha wale waliokuwa hawana leseni walitunukiwa vyeti vitakavyo wasaidia kupata leseni.

Lengo kuu la mafunzo hayo, lilikuwa ni kupunguza tatizo la ajali za barabarani zinazopoteza mamia ya watanzania kila mwaka na hata wengine kubaki na ulemavu wa kudumu.

Hili la kuwapatia mafunzo hayo madereva halikuja bahati mbaya, bali ni baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo kuona ipo haja ya madereva kupatiwa elimu ili waweze kusafiri na kusafirisha abiria salama.

Madereva waliofanikiwa kupata elimu hiyo wanaishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Mpogolo kuhakikisha wanapatiwa elimu wakibainisha wamevijua vitu vingi vipya vinavyohusisha Sheria za barabarani.

Msemaji wa Shirikisho la Madereva wa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam, Tito Lazaro ambaye ni miongoni mwa waliohudhuria mafunzo hayo anasema ilikuwa ni muhimu kwa sababu kila siku madereva wapya wanaingia wengi kuliko wanotoka.

Anasema Mpogolo alitoa siku 30 kwa madereva wa guta za umeme ambazo zilikuwa hazina namba za usajili ili madereva wake wawe na leseni ya udereva lengo ilikuwa wapete elimu kisha wapewe vyeti vitakavyo wasaidia kupata leseni.

“Tulipewa mafunzo ya siku 14 bada ya hapo madereva tulipatiwa vyeti na kwa wale waliokuwa hawana leseni watavitumia kupata leseni lakini muhimu zaidi sasa tunafuata sheria na hali ya usalama barabarani kila siku inazidi kuimarika katika mkoa wa Dar es Salaam.

Anasema madereva wengi wanazidi kuimarika kwa kutambua sheria na kwamba kwa sasa unaweza kutoka Mwenge mpaka Gongo la Mboto bila kushuhudia ajali tofauti na miaka ya nyuma lilikuwa jambo lisilo wezekana.

Anasema licha ya kupatiwa mafunzo hayo, Jeshi la Polsi limekuwa likitoa elimu kwa madereva hao kwa kuwafuata mahali wanakoegesha vyombo vyao na hata wakati mwingine kutumia vyombo vya habari.

Dereva mwingine aliyepata mafuno hayo, Juma Hamisi anasifu yalikuwa mazuri na amevijua vitu vingi katika mafunzo hayo ikiwamo maana ya zile alama za barabarani.

Hata hivyo, Hamisi anawasilisha ombi kwa serikali kwamba mafunzo hayo yawe endelevu ili ambao hawakupata elimu hiyo waipate kulisaidia taifa kuondokana na ajali zinazoweza kuzuilika.

“Ninamshukuru Mpogolo kwa maono yake, na kwa moyo wake kujali na kutusikiliza wakati wote tunapokuwa na shida katika ofisi yake” anasifu

1


WENYE MAGUTA WAFIKIWA

Kutokana na kuwapo kwa wimbi la madererava wa maguta yanayotumia mfumo wa umeme waliokuwa wanaendesha bila kuwa na namba za usajili jambo liliokuwa linawafanya wasiwe na leseni Mpogolo akatoa siku 30 kuhakikisha wanasajiliwa na wanapatiwa mafunzo ili waweze kuwa na leseni.

Mwenyekiti wa Toyo za Umeme, Hamza Amri anasema walipata mafunzo yaliyogusa masuala ya sheria na kanuni za barabarani na madereva zaidi ya 400 walihudhuria.

“Tulifurahi kupata mafunzo hayo, na ushirikiano aliotupa Mpogolo kupata mafunzo hayo, kwa madereeva wa maguta hali kwa sasa baada ya mafunzo inaridhisha.

“Pale mwanzo kwa mfano njia za katikati ya jiji kuna alama zilikuwa zinaonesha njia fulani haitoki tulikuwa hatujui lakini sasa tukiziona tunajua zinamaanisha nini.

“Lakini pia kwa sasa madereva wamekuwa wastaarabu hata lugha za mdomoni mwao zimebadilika, tumefunzwa kuwa barabara ni ya wote mwanzo ilikuwa tunasimama hata katikati ya barabara tunapakia abiria laikni saizi hakuna hali hiyo tena. Tulikuwa hatujui sheria za usalama barabarani zina mafungu mangapi lakini sasa tunajua yapo matano.
2


WALICHOOMBA

Kiongozi huyo, anasema siku hiyo walimuomba Mpogolo kungalia uwezekano wa betri na mota za maguta hayo zishuke bei kwa kuwa kwa sasa betri zinauzwa Sh 800,000 kwahiyo likiharibika madereva wanashindwa kumudu gharaa kununua jipya.

Pia walishauri Shirika la Viwango Tanzania (TBS) bidha hizo zinapoingia nchini zikaguliwe ubora wake ili kuwapunguzia wananchi hasara kwa kununua vitu vibovu.

“Kwa mfano wenzetu wa bodaboda wanalalmika kuhusu (helmenti) kofia ngumu ikianguka tu chini inapasuka sasa hiyo haiwezi kuwa kofia ngumu wala kumsaidia akipata ajali” alisema  

Pia aliomba wapatiwe maeneo maalumu ya maegesho yatakayokuwa rafiki na shughuli zao lakini wakajibiwa na Mkurugenzi wa jiji hilo, Elihuruma Mabelya kwamba suala hilo linafanyiwa kazi.Na maegesho imependekezwa iwe Sh 500 kwa siku.

ASEMAVYO DC

Mpogolo anapofunga mafunzo hayo kwanza anaanza kwa kuwashukuru madereva hao kujitokeza kupatiwa mafunzo akisifu jambo hilo litasaidia kupunguz ajali za barabarani.

Anasema dereva anapopata cheti na kusajiliwa anakuwa mtu muhimu katika jamii na ni lazima wajisajili ili iwe rahisi kutambulika hata kuaminiwa kupeleka mizigo mahali fulani.

“Ni kwa sababu ya usalama wa Mali za watu ukijisajili yule anayekupa mzigo atakuamini atakwambia peleka mbezi maana yeye sio lazima aende huko na pia itasaidia kukuza uchumi wa nchi yetu” anasema Mpogolo

Kuhusu ombi lao la betri kuuzwa kwa gharama kubwa anasema atalifikisha kwa Rais Samia ili aangalie namna ya kuwasaidia kwa kuwa ni msikivu sana na kwamba vijana wakimtumia vizuri watanufaika naye.



“Dunia nzima inamtambua Rais Samia kama ‘champion’ wa mazingira na kwa kutumia bajaji za umeme betri ili kuepuka uchafuzi wa mazingira ni jambo zuri zaidi kwake tuna wajibu wa kumsadia zipatikane kwa bei nzuri ili kusaidia kutunza mazingira” anasema Mpogolo huku akishangiliwa na madereva hao na kuongeza  

“Ule usemi wa ombeni nanyi mtapewa, umedhihirisha usikivu wa Rais Samia kapunguza gharama za lesini kwa maafisa usafirisha wa bodaboda, bajaji na guta zinazotumia umeme katika bajeti ya mwaka 2025-2026 kulipia kiasi cha Sh 30,000” anasema Mpogolo

mpogolo anasema usikuvu wa Rais Samia umeendelea kuhakikisha vilio vya madereva wa vyombo vya moto vinasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani.

Hata hivyo Mpogolo, anaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vijana walionufaika na mafunzo hayo kutoka maeneo mbalimbali kufanya shughuli zao vizuri katikati ya jiji kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu watazowekewa ili kupunguza msongamano katika masoko.

Anatumia nafasi hiyo kuwakumbusha vijana kutumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi, ili waweze kusaidia familia zao na kutoa mchango wa maendeleo kwa serikali, kwa kuwa kazi ni msingi wa utu.

“Hiki mlichokifanga kinaenda kuboresha uchumi wa kwako familia na aliyenunua chombo mwisho uchumi ni wa nchi yetu unakuwa.  

“Sambamba na kuchangia kwa ukuaji wa uchumi manaenda kupata ajira rasmi kwa sababu mnakuwa madereva wenye leseni na mliopata mafunzo” anasema

3