WIKI YA AFYA; Madaktari bingwa waongezeka, magonjwa tishio yadhibitiwa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:41 PM Apr 09 2025
Mchoro
Mchoro: Christina Mwakangale
Mchoro

MIAKA minne ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afyaimekuwa kielelezo cha mafanikio ya utawala wake ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya ya jamii na kulinda nguvu kazi ya taifa.

Katika kipindi hicho, vifo vitokanavyo na magonjwa matatu ambayo ni malaria, kifua kikuu pamoja na

Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) vimepungua sawa na ilivyo kwa vifo vitokanavyo na uzazi, huku madaktari bingwa na vifaa tiba katika hospitali nchini wakiongezeka.

Wakati hayo yanajiri, Wizara ya Afya nayo ikaamua kutenga wiki ya afya nchini ambayo iliadhimishwa kuanzia Aprili 3 hadi 8 mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza, lengo likiwa ni kukuza uelewa kwa umma kuhusu masuala ya afya ambayo ndio ustawi wa jamii.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama
Mwandishi ameangazia vyanzo kadhaa, likiwamo Jarida la Afya la Wizara ya Afya kuanzia hatua ambazo nchi imepiga kukabiliana na baadhi ya magonjwa na kukua kwa utaalamu katika tiba.

Kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, inaelezwa na Wizara ya Afya kuwa asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilomita tano ya maeneo yao wanamoishi, huku lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030.

MALARIA

Ugonjwa wa malaria kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023, vifo vilipungua kutoka 1,882 mwaka 2021 hadi 1,540 mwaka 2023.

Serikali pia imeendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo. Mwaka 2023 watu milioni 19.8 walipimwa malaria, waliokutwa na maambukizi ni milioni 3.46.

Mwaka 2022, watu milioni 18.6 walipimwa malaria. Kati yao, milioni 3.52 walikutwa na maambukizi.

Mwaka 2021 watu milioni 20.241,982 walipimwa, milioni 4.4 walikutwa na maambukizi.

KIFUA KIKUU

Kuhusu kifua kikuu, takwimu zinaonyesha maambukizi ya ugonjwa huo yamedhibitiwa. 

Mwaka 2023, watu 440,988 walipima kulinganishwa na watu 398,676 waliopimwa mwaka 2022 na 354,324 waliopimwa mwaka 2021.

Majibu ya taarifa hiyo yalionesha kuwa waliogundulika kuugua ugonjwa huo mwaka 2023 ni 90,585 kulinganishwa na watu 100,984 mwaka 2022 na watu 60,068 mwaka 2021.

Mwaka 2023, vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vilipungua vikiwa 18,100 kulinganisha na mwaka 2022 vilipokuwa 25,800 na mwaka 2021 vilikuwa 26,800.

VVU/ UKIMWI

Katika miaka minne, udhibiti wa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) yalipungua. 

Mwaka 2023 watu 8,145,576 walipima maambukizi ya ugonjwa huo kulinganishwa na watu 6,930,758 waliopimwa mwaka 2022 na 6,493,583 waliopima mwaka 2021. Hii ni kwa kwa mujibu wa taarifa kutoka Mfumo wa DHIS 2023.

Majibu yalionyesha kuwa kati ya watu 163,131 walingundulika kuwa na maambukizi ya VVU mwaka 2023 ukilinganisha na watu 182,095 waliogundulika mwaka 2022 na watu 198,042 mwaka 2021.

Takwimu pia zilionyesha kuwa wagonjwa waliokuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV), waliongezeka na kufikia 1,663,651 hadi Desemba 2023 kulinganisha na watu 1,612,512 waliotumia dawa hizo hadi Desemba 2022 na watu 1,520,589 mwaka 2021.

Vifo vitokanavyo na UKIMWI vilipungua. Mwaka 2023 vilikuwa 22,000 kulinganishwa na vifo 29,000 mwaka 2022 na vifo 25,000 mwaka 2021 (Spectrum 2022).

Hadi kufikia Desemba 2023, idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya tiba na matunzo vimefikia 7,396 kutoka 7,072 mwaka 2021 na kati ya hivyo CTC kamili ni 3,572.

HUDUMA ZA DHARURA

Kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021, serikali imekamilisha ujenzi wa majengo 23 ya kutoa huduma za dharura katika hospitali maalum, kanda na mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba.

Wateja 262,260 wamenufaika na huduma za dharura nchini na kuokoa maisha kwa wagonjwa wa dharura na wa ajali kwa asilimia kati ya 40 na 50 kwa mujibu wa utafiti za kitaalam.

VITUO HUDUMA

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021, umefanyika uwekezaji katika miundombinu ya kutolea huduma za afya na vituo vya afya vimeongezeka kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi 9, 610 Machi 2024 sawa na ongezeko la vituo 1,061.

Vilevile, katika miaka minne kumefanyika maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano.

Maboresho hayo yamegharimu Sh. trilioni 1.02 na yalifanyika katika ukarabati wa majengo ya zamani na kuendelea na ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa.

WATAALAMU

Katika miaka minne, serikali imeendelea kuajiri wataalam katika sekta ya afya, ambapo wataalam 35,450 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. 

Ajira za mikataba kwa watumishi wa afya 2,836 kupitia miradi mbalimbali ya serikali zilitolewa. Pia kumekuwa na ongezeko la madaktari bingwa na bobezi nchini kutoka 805 mwaka 2020 hadi 2,464 mwaka 2023.

VIFO UZAZI

Vifo vitokanavyo na uzazi kwa wajawazito vimepungua kwa asilimia 80 kutokana na kuimarika kwa huduma za uzazi, mama na mtoto vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa.

Kadhalika, huduma za bingwa na bobezi zinapatikana nchini kwa gharama nafuu katika kipindi cha miaka mitatu, huduma za ubingwa bobezi zilizotolewa zilikuwa ni pamoja na upandikizaji vifaa vya usikivu kwa watoto, upandikizaji figo na upandikizaji uloto.

Pia upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo wagonjwa 5,954 kati yao wagonjwa 2,289 wamefanyiwa katika kipindi cha mwaka 2023/24.

Wagojwa waoliwekewa goti bandia walikuwa 662. Waliowekewa puto tumboni hadi sasa ni 200.

TIBA KIBOBEZI

Kufungwa kwa vifaatiba vya kisasa, kuwapo watalaam, dawa na maabara za kisasa zenye vifaa na vitenganishi, dawa na vitendanishi katika hospitali kubwa za umma ikiwamo Hospitali ya

Taifa Muhimbili (MNH), kumeiweka Tanzania kwenye ramani ya nchi zinazotoa huduma za kibingwa na bobezi.

Katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), kumefungwa vifaa vya kisasa vya kitabibu (endoscopic tower), ikiwamo ya ubongo (Neuro Microscope), zinazowezesha matabibu kufanya upasuaji kwa njia ya matundu.

Kufungwa kwa mashine hizo kumesaidia upasuaji kufanyika kupitia tundu dogo badala ya madaktari kufungua fuvu au sehemu kubwa.

Taasisi hiyo ina mashine mbili za MRI zenye uwezo wa 1.5T, hivyo kubaini tatizo kwenye mishipa ya ubongo na kwenye fuvu.

Vilevile, kuna CT Scan yenye uwezo wa vipande 128, inayoweza kupiga picha mwili mzima wa binadamu na kubaini tatizo ndani ya sekunde kadhaa.

Mashine hiyo pia inatumika kutambua na kufuatilia hali mbalimbali za matibabu. 

MOI pia ina maabara ya upasuaji na uchunguzi wa ubongo, mashine ya upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu, upasuaji magoti na mabega kwa njia ya matundu, upasuaji ubongo kupitia tundu la pua na upasuaji kwa njia ya matundu watoto wanaozaliwa na tatizo la kichwa kikubwa.

Kwa upande wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Tanzania imejiimarisha kwenye uchunguzi na tiba, mashine ya PET-CT scan inayoweza kubaini kwa haraka hatua ya ugonjwa kwa kila mgonjwa imesimikwa.

Mashine hiyo inayotumika katika kutambua ugonjwa wa saratani uko katika hatua gani na inatoa mwanga kwa mtaalam wa afya kupanga matibabu sahihi kulingana na hatua ya mgonjwa.

Pia ina uwezo wa kufanya uchunguzi ndani muda mfupi, kutoa picha za kina za mwili, kutambua ugonjwa, kupanga matibabu na kufuatilia ufanisi wa tiba.

MUHIMBILI

Kwa upande wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inatoa huduma za kibingwa na kibobezi kama upandikizaji figo, upasuaji wa kisasa kwa kutumia tundu dogo, upasuaji rekebishi, upandikizaji mimba na huduma bingwa za uzazi.

Kuna mashine ya kisasa inayoitwa bronchoscopy yenye uwezo wa kutambua na kutibu matatizo ya mapafu na njia ya hewa.

Uwezo wa hospitali hiyo imeiwezesha Tanzania kupokea wagonjwa 7,576 kutoka Comoro,

Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Zambia na Msumbiji waliofika kutibiwa.