Msafara wa Twende Butiama umetoa misaada kwa shule nne za msingi zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Singida mkoani hapa.
Misaada hiyo iliyokabidhiwa jana kwa shule hizo za za Minga, Tumaini, Unyankindi na Somoku ni pamoja na magodoro, vitanda, shuka, meza kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, viti vya darasani, viti mwendo na miche 100 ya miti.
Mwenyekiti wa Twende Butiama, Gabriel Landa, akikabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Manispaa hiyo, Omary Maje, alisema kila mwaka wamekuwa wakitoa misaada katika mikoa mbalimbali wakati wa msafara huo wa baiskeli.
Alisema msafara huo ulianzia Julai 3, mwaka huu jijini Dar es Salaam na unatarajia kuhitimishwa jumapili wiki hii katika KIjiji cha Butiama Wilaya Musoma mkoani Mara, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Landa aliwataja washiriki wengine katika msafara huo kuwa ni raia utoka nchi jirani za Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi Congo (DRC), Burundi na Uganda.
Alisema msafara huo ni njia mojawapo ya kumuenz Nyerere ambaye urithi wake wa fikra na maono unaendelea kuiongoza Tanzania.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, msafara huo umetoa mafanikio makubwa ikiwemo kupanda miti zaidi ya 100,000, kufikia watu 23,000 kupitia huduma za afya kwa njia ya kliniki tembezi, kugawa madawati 1,900 kwa shule 32 za umma na kutoa baiskeli 50 kwa wanafunzi waishio mbali na shule.
Mmoja wa wahisani wa msafara huo, Chiha Nchimbi, alisema misaada hiyo ina lengo la kukabiliana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni ujinga, umaskini na maradhi kama alivyokuwa akisisitiza na Nyerere wakati wa uhai wake.
Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Manispaa hiyo, Omay Maje, aliushukru msafara huo kwa sasa huo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kutatua changamoto katika sekta ya elimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED