Waziri Mkuu kufungua Umisseta, Umitashumta

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:49 AM Jun 03 2025
Waziri Mkuu kufungua Umisseta, Umitashumta
Picha: Mtandao
Waziri Mkuu kufungua Umisseta, Umitashumta

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufungua michuano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari (Umisseta) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) yenye lengo la kuimarisha afya na ndoto zao itakayoanza Juni 7 hadi 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Yusuf Singo, imeeleza kuwa mwenyeji wa michezo hiyo ni Mkoa wa Iringa, ambapo itakuwa ni fursa ya kuonesha vipaji katika taaluma, kukuza vipaji, kuimarisha maadili na kuandaa taifa imara la kesho.

“Michezo hiyo watachuana vikali kuonesha vipawa katika taaluma, sanaa na michezo mbalimbali na itakuwa fursa ya kulea vijana kama viongozi wa kesho,” alisema Singo.

Aidha, alisema katika michezo hiyo mashindano ya sanaa na michezo yatapewa kipaumbele ikiwamo ngoma za asili, kwaya na muziki wa kizazi kipya (Bongo Flavor) ni sehemu ya fani ambazo zimekuwa zikishindaniwa Umisseta.

Singo alisema kupitia sanaa na michezo, wanafunzi wanapata nafasi ya kuonesha vipaji vyao katika kucheza ngoma zenye asili ya makabila ya mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kizalendo na kuburudisha kupitia muziki wa kizazi kipya.