KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amesema timu yake "ina matatizo mengi" baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspur.
Bao la kusawazisha la Matthijs de Ligt dakika ya 96 liliokoa pointi kwa United na kuendeleza mbio zao za kutopoteza hadi mechi tano, ambayo ni rekodi kwa kocha huyo wa Ureno, lakini alikiri kuwa timu yake ilirudia makosa kama ilivyokuwa kwenye sare ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Nottingham Forest.
United waliongoza kwa muda mrefu kupitia kwa bao la Bryan Mbeumo aliyefunga kwa kichwa kipindi cha kwanza, lakini mabao ya kutoka kwa mchezaji wa akiba wa Spurs, Mathys Tel na Richarlison, yaligeuza mchezo kabla ya De Ligt kufunga dakika za majeruhi kusawazisha.
Amorim alisema United, ambao wangeshika nafasi ya pili kama wangeibuka na ushindi kwenye mchezo huo, walijitahidi kuvumilia alipowatoa Casemiro na Harry Maguire zikiwa zimesalia dakika 20.
"Tuna matatizo mengi," alisema Amorim akiwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo.
"Najua wakati mwingine matokeo yanaonesha kwa watu kwamba, tunaboresha, lakini tuna mengi ya kufanya.
"Unaweza kugawanya mchezo katika dakika 10 za mwisho, pia tunapolazimika kuwatoa Harry Maguire na Casemiro kwa wakati mmoja, kisha tupate mabao mawili.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED