Arusha Sports Complex kufungua milango vilabu vikubwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:06 PM Jun 19 2025
Arusha Council Sports Complex.
Picha: Mpigapicha Wetu
Arusha Council Sports Complex.

Halmashauri ya Jiji la Arusha, limetangaza kuanza rasmi kwa ujenzi wa uwanja wake mpya wa kisasa wa mchezo wa mpira wa miguu utakaoitwa Arusha Council Sports Complex.

Uwanja huo utakaokuwa na uwezo wa kuchukuwa watazamaji waliokaa vitini  8,000, hadi kukamilika kwake utaigharimu Jiji hilo zaidi ya Sh. bilioni 9.614

Jana, Juni 18, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dk. Nindwa Maduhu, akizungumzia mradi huo, wakati wa utiaji saini mkataba wa kuanza kwa ujenzi huo, kati yake na Kampuni ya STC Construction Limited na Halmashauri ya Jiji la Arusha, amesema uwanja huo, pia utakuwa na viwanja vya michezo ya netiboli, kikapu na tenisi.

Amesema uwanja huo, utakuawa na vyumba vinne vya kubadilishia nguo, ofisi nane, ukumbi wa watu mashuhuri, malango 12 na taa kwa ajili ya kuchezwa kwa michezo usiku.

Kwa mujibu wa Dk.Nindwa, uwanja huo utazungukwa na maduka 98 pamoja na maegesho ya magari 150.

Akishuhudia kusainiwa kwa mkatana huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, amesema kwa muda mfupi jiji hilo litakuwa na viwanja vya kisasa saba.

Alisema viwanja hivyo ni pamoja na mkubwa zaidi utakaochukuwa watu zaidi ya 30,000 utakaotumika kwa ajili ya michuano ya kombe la  mataifa ya Afrika (AFCON-2027).