Carlo Ancelotti aaga rasmi Real Madrid kwa barua ya hisia kwa mashabiki

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:11 PM May 27 2025
 Carlo Ancelotti aaga rasmi Real Madrid kwa barua ya hisia kwa mashabiki
Picha:Mtandao
Carlo Ancelotti aaga rasmi Real Madrid kwa barua ya hisia kwa mashabiki

Aliyekuwa kocha wa Real Madrid kwa vipindi viwili tofauti, Carlo Ancelotti, ametuma ujumbe wa barua wa kuwaaga mashabiki wa klabu hiyo, akieleza hisia zake na shukrani baada ya kumaliza rasmi muda wake wa pili wa kuifundisha timu hiyo.

Ancelotti alihudumu kama kocha wa Real Madrid kwa mara ya kwanza kuanzia Juni 25, 2013 hadi Mei 25, 2015, na kisha kurejea tena Juni 1, 2021 hadi Mei 2025. Katika ujumbe wake wa kuaga, Ancelotti aliandika:

“Leo tunaenda tofauti tena. Leo tena naweka moyoni mwangu kila wakati niliishi katika hatua hii nzuri ya pili kama kocha wa @RealMadrid.”“Imekuwa miaka isiyoweza kusahaulika, safari ya ajabu iliyojaa hisia, mataji, na, zaidi ya yote, fahari ya kuwakilisha nembo hii.”

Kocha huyo mkongwe alitoa shukrani kwa rais wa klabu Florentino Pérez, wachezaji, benchi lake la ufundi, na zaidi ya yote, mashabiki wa Real Madrid aliowataja kuwa wa kipekee kwa kumuunga mkono kila hatua.

“Tulichofanikiwa pamoja kitabaki milele katika kumbukumbu ya Madridismo... si kwa ushindi pekee, bali kwa namna tulivyofanikiwa. Usiku wa ajabu wa Bernabéu sasa ni sehemu ya historia ya soka.”

Ancelotti alihitimisha ujumbe wake kwa kusema:

“Sasa tukio jipya linaanza, lakini uhusiano wangu na @RealMadrid ni wa milele. Tutaonana hivi karibuni, Wana Madridistas! Hala Madrid Y Nada Más!”

Licha ya mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kushinda mataji kadhaa ya ndani na kimataifa, Real Madrid ilitangaza rasmi tarehe 23 Mei 2025 kuwa Ancelotti angeondoka klabuni mwishoni mwa msimu huo. Nafasi yake sasa inachukuliwa na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Xabi Alonso, ambaye pia aliwahi kufundisha timu za Real Madrid B na Bayern Munich.