Gamondi alalamikia uwanja

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:38 PM Nov 10 2025
news
Picha Mtandao
Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi.

BAADA ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi ameulalamikia Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuwa ndiyo uliowakosesha ushindi.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo juzi, Gamondi alisema haikuwa rahisi kucheza kwenye uwanja huo kwa sababu haikuwa kwenye hali nzuri, hivyo wachezaji wake walilazimika kupiga mipira mirefu kitu ambacho si aina yao ya uchezaji.

"Kwangu mimi naona haikuwa rahisi sana kucheza vizuri na kushinda kwenye uwanja kama huu, tulishindwa kucheza tukaamua kupiga mipira mirefu ambapo si staili yetu,” alisema Gamondi.

“Ni ngumu sana kucheza hapa kwa sababu utakiwi kukimbia sana na kupiga mipira mirefu na si pasi fupi. Kipindi cha kwanza tulicheza vizuri, lakini hatukufanikiwa kutengeneza nafasi nyingi.

Kiungo mshambuliaji, raia wa Zambia, Clatous Chama, alifunga bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu akiwa na Singida Black Stars kipindi cha kwanza, kabla ya Kelvin Nashon kusawazisha kipindi cha pili na kuzifanya timu hizo kugawana pointi moja.