TIMU zimejipanga, hayo ni maneno ya Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally kuelekea mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal United itakayochezwa Februari 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kocha huyo alisema kikosi chake kinaendelea kujipanga kwa sababu anaenda kukutana na Coastal Union iliyoimarika.
Alisema mechi zote za mzunguko wa pili huwa na ushindani kwa sababu timu zimerekebisha makosa na zimeimarisha vikosi kwa kuongeza wachezaji wapya wakati wa dirisha dogo.
"Niseme tu Coastal Union ambayo iko chini ya Mwambusi (Juma), imeimarika, sio ile, tunajiandaa vyema kuikabili, hautakuwa mchezo mwepesi," alisema kocha huyo.
Winga wa timu hiyo, Shiza Kichuya, alisema wachezaji wote wamejipanga kusaka matokeo chanya na wanaamini hilo linawezekana.
"Tuko tayari kwa mechi hiyo, tumefanya maandalizi mazuri, ninaamini kama tutafuata maelekezo vyema, kokote unapata ushindi, tunaenda kupambana ili turudi na pointi tatu muhimu," Shiza alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, JKT Tanzania yenye pointi 19 iko katika nafasi ya nane huku Coastal Union yenye pointi 18 iko kwenye nafasi ya 11, KenGold ya Mbeya inaendelea kuburuza mkia ikiwa na pointi sita kibindoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED