Mabedi: Yanga itapindua meza

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango ,, Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 12:22 PM Oct 21 2025
news
Picha Mtandao
Mchezaji wa klabu ya Yanga Mzize Clenent.

BAADA ya kushuhudia timu yake ikipata kipigo cha bao 1-0 ugenini mbele ya Silver Strikers ya Malawi, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Patrick Mabedi, amesema timu yake hiyo bado ina nafasi ya kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na itapindua meza katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Jumamosi wiki hii.

Yanga Jumamosi iliyopita ilikumbana na kipigo hicho kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Bingu Mutharika mjini LIlongwe, Malawi, kipigo ambacho kimemfukuzisha kazi aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Roman Folz.

Mabedi, alisema kikosi chake bado kina nafasi ya kusonga mbele na watayafanyia kazi yale waliyoona yaliwakwamisha kuweza kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Alisema mchezo wa marudiano utakuwa muhimu zaidi kwao kwa kuwa watacheza nyumbani mbele ya mashabiki wao huku lengo likiwa kuvuka hatua hiyo na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

"Tuna dakika 90 nyingine..., mashabiki hawapaswi kukata tamaa, tunajipanga kwa mchezo wa marudiano ambao tutakuwa nyumbani..., kwa siku chache zilizobakia tutafanyia kazi yale ambayo tumeona yamechangia sisi kupoteza mchezo ule, tutarejea uwanjani na hali kubwa na uchu wa kusonga mbele, nafasi ya kufanya hivyo bado ipo," alisema kocha huyo raia wa Malawi.

Alisema mchezo huo wa marudiano kitu pekee wanachokihitaji ni ushindi mzuri kuweza kusonga mbele na kuingia hatua ya makundi ya michuno hiyo.

Ili kusonga mbele, Yanga wanahitaji ushindi wa angalau mabao 2-0 kuweza kuwatupa nje ya mashindano mabingwa hao wa Malawi wa msimu uliopita.

Utayari huo wa Yanga unaungwa mkono na Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Dikson Job, ambaye amesema bado haujaisha.

"Wenzetu wapo mbele kwa bao moja, tuna dakika nyingine 90 za kupambania timu yetu kuingi hatua ya makundi, mashabiki wetu wajitokeze tu kwa wingi siku ya mchezo wa marudiano, na naamini hatutawaangusha kwenye ardhi ya nyumbani," alisema Job.

MZIZE AANDALIWA KUIMALIZA

Wakati huo huo, jopo la madaktari wa Yanga, likiongozwa na Moses Etutu, limethibitisha kuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Clement Mzize, hana tena changamoto iliyokuwa inamkabili, hivyo anaruhusiwa kurejea uwanjani.

Etutu amesema jana kuwa, Mzize yuko fiti kwa asilimia 80, ambapo hadi mwishoni mwa wiki hii, atakuwa na utimamu wa mwili kwa asilimia 100, huku akiwa ameshapona jeraha lake.

"Kwa sasa yuko salama, ni mzima kwa asilimia 80, tunaamini katika mchezo ujao, nafasi ya yeye kucheza ni kubwa sana, hapo sasa tunayemwachia ni kocha, lakini sisi tumeshamruhusu kufanya hivyo.

Ameshatoka kwenye mazoezi ya peke yake, hivi sasa amejiunga na wenzake, tunategemea mwishoni mwa wiki atakuwa fiti kwa asilimia 100," alisema daktari huyo.

Hii ni baada ya mastraika wengine, Andy Boyeli na Prince Dube, kushindwa kutumbukiza mipira wavuni katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa, Jumamosi iliyopita.

UONGOZI WALIA NA KIWANGO

Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison, ameliambia gazeti hili jana kuwa, licha ya kutoridhishwa na kiwango cha timu hiyo, yaliyotokea kwenye mchezo uliopita yamepita na sasa wanaangalia mechi ijayo. 

Alisema baada ya kumaliza mchezo wao wa awali waliendelea kusalia Malawi wakifanya mazoezi ili kuimarisha zaidi miili ya wachezaji kabla ya kurejea nchini. 

"Jumanne ( leo), timu yetu itaingia kambini rasmi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu wa marudiano, nafahamu mashabiki wamekatishwa tamaa na matokeo yaliyopita, tuyasahau na badala yake tuelekeze mawazo yetu kwenye mchezo wetu wa Jumamosi," alisema Harrison. 

Alisema anaamini watapata ushindi katika mchezo huo na  kuweka historia ya kuingia hatua ya makundi wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani.