MSHAMBULIAJI Fiston Mayele, ameweka rekodi yake Ligi ya Mabingwa Afrika huku akiiwezesha pia klabu yake ya Pyramids kuandika historia mpya katika mashindano hayo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani humu.
Mayele alikuwa mchezaji muhimu kwa Pyramids kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika juzi baada ya kufunga bao la kuongoza kwenye mchezo wa fainali ya mkondo wa pili dhidi ya Mamelods Sundowns, wakishinda mabao 2-1 nchini Misri juzi na hivyo kubeba taji hilo kwa ushindi wa jumla wa 3-2, kutokana na fainali ya mkondo wa kwanza nchini Afrika Kusini kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea Yanga, amemaliza michuano hiyo kwa kutwaa Kiatu cha Dhahabu, kutokana na kuwa kinara wa ufungaji akiwa na mabao tisa akifuatiwa kwa mbali na mchezaji mwenzake, Ibrahim Adel mwenye mabao sita, Imam Ashour wa Al Ahly (mabao 4), Lucas Ribeiro Costa kutoka Mamelodi Sundowns (mabao 4) na Peter Shalulile wa Mamelodi Sundowns (mabao 3).
Mayele, pia anakuwa mchezaji wa pili kutoka DR Congo ndani ya kipindi cha miaka 10, kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Kocha wa Pyramids, Krunoslav Jurcic, pia ameandika historia kwa kuwa Mcrotia wa kwanza kuiongoza timu kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kuwa miongoni mwa makocha kutoka barani Ulaya waliowahi kushinda taji hilo la Afrika.
Wengine waliowahi kutwaa taji hilo ni pamoja na Ivan Ridanovic na Branko Zutic kutoka Yugoslavia, miaka mingi iliyopita.
Ushindi huo ni fahari kubwa kwa Pyramids FC, kwani ni mara ya kwanza kwao kutwaa taji hilo tangu klabu hiyo ilipoanzishwa miaka 10 iliyopita. Na kwa Misri hiyo ni fahari kubwa kwa nchi yao kwani sasa timu zao zimetwaa taji hilo kwa miaka mitatu mfululizo.
Al Ahly ilitwaa ubingwa huo mwaka 2023 na 2024. Hii ikionesha kuwa Misri bado ipo juu kisoka kwa nchi za Afrika kwani ni mfululizo wa kiwango bora kwa klabu zao.
Kwa Mamelodi Sundowns, ulikuwa ni usiku mgumu kwao wakati ikiwa na matumaini ya kushinda taji lao la michuano ya CAF kwa mara ya pili, lakini pia kipigo hicho kikija kwao wakati ikitaka kuichapa timu ya kwanza fainali baada ya kuitundika Al Ahly mwaka 2012 kwenye mechi ya fainali nyumbani.
Mbali ya bao la kwanza la Pyramids ambalo lilifungwa dakika ya 23 na Mayele, lingine liwekwa nyavuni dakika ya 56 na beki Ahmed Samy akiunganisha nyavuni kwa kichwa krosi ya Mohamed Chibi, huku lile la Mamelodi Sundowns likizamishwa kimyani dakika ya 75 na Iqraam Rayners.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED