Mligo aanika siri alivyoiteka Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:07 AM Nov 06 2025
news
Picha Mtandao
beki mpya wa Simba, Antony Mligo.

HUKU wakijiandaa kuikabili JKT Tanzania, beki mpya wa Simba, Antony Mligo, amesema ‘siri kubwa’ ya kupata namba ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi na kuziba vyema nafasi iliyoachwa na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' ni kujituma mazoezini, kujiamini na kufahamu kilichompeleka katika klabu hiyo.

Mligo, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Namungo FC, amewaambia wanachama na mashabiki wa Simba alichokitoa mpaka sasa ni kidogo kwa sababu hajakuwa katika kiwango chake anachokifahamu, akiahidi watafurahi zaidi siku za baadaye.

Beki huyo aliwashukuru wanachama na mashabiki wa Simba ambao wameonekana kumkubali licha ya kucheza kwa muda mfupi na michezo michache.

"Namshukuru sana mwenyezi Mungu kwa mwanzo huu mzuri ambao nimeanza, hizi ni asilimia chache sana ambazo nimezionesha, kuna mambo mazuri mengi yanakuja. Bado kwa sasa nina ugeni, ninachezea timu kubwa yenye mashabiki wengi, hiyo bado kidogo inaleta shida.

Pamoja na hayo nawashukuru mashabiki wamenikubali sana kwa maana hiyo,  nina deni kubwa kwao kwa kuniamini kiasi hiki, wamenifanya niendelee kujiamini na kuipambania nembo ya klabu, pamoja na yangu mwenyewe niliyojiwekea," alisema mchezaji huyo.

Wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameonekana kumkubali Mligo na mapema kuanza kumsahau aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Zimbwe Jr, aliyetimkia kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.

Mchezaji huyo alisajiliwa kwa mbinde, ukiwa ni ushawishi wa kocha wa zamani, Fadlu Davids, ambaye aliamua kulivalia njuga suala la usajili wake, ambapo awali baadhi ya viongozi wa Simba hawakutimiza matakwa yake.

Wakati Fadlu akimhitaji mchezaji huyo baada ya kuvutiwa naye akionesha kiwango bora katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu akiwa na Namungo, viongozi walimsajili, Miraji Athumani, wa Coastal Union.

Hata hivyo, Fadlu, alipinga usajili huyo na baadhi ya waliokuwa karibu yake walidai alifikia wakati akasema hata kama hakusajiliwa na klabu, atatoa fedha yake ‘mfukoni’ kumsajili Mligo, kitu ambacho kilifanya viongozi waanze kuhaha na kufanikiwa kumnasa beki huyo.

Kuondoka ghafla kwa Fadlu, raia wa Afrika Kusini kulionekana huenda angekaa benchi kutokana na ujio ya mwalimu mpya, Dimitar Pantev, lakini Mligo alizidi kusimika nafasi yake kufuatia kiwango bora alichokionesha kwenye mchezo yote ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amecheza michezo yote sita ya mashindano, minne ya Ligi ya Mabingwa, hatua za awali dhidi ya Gaborone United ya Botswana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, pamoja na miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate na Namungo.