WAKATI wanachama na mashabiki wa Simba wakifurahia kiwango kilichooneshwa na wachezaji wao juzi nchini Eswatini na kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya huko, Meneja Mkuu, Dimitar Pantev, amesema kwa upande wake hajaridhishwa na kiwango cha soka katika mchezo huo, japo anaona vijana wake wanaonesha mwanga wa kuelekea kuwa tishio.
Simba, ikiwa Mbabane kwenye Uwanja wa Somhlolo, ilipata ushindi huo katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, ikibakisha kazi moja tu ya kuulinda ushindi wake, itakapocheza, Jumapili wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya ushindi huo katika hatua ya raundi ya kwanza, uliowapagawisha mashabiki wa Simba pamoja na kiwango kilichooneshwa na wachezaji, walionekana kubadilika tofauti na mechi zilizopita, lakini kocha Pantev, amesema katika mchezo huo alichofurahia ni matokeo tu, lakini si kiwango.
"Matokeo ni mazuri sana tuliyoyapata, ila tukiongelea kiwango cha soka bado sina furaha nacho, tunatakiwa tufanye kazi ya ziada kama tunataka kwenda mbali sana kwenye michuano hii.
"Kipindi cha kwanza wachezaji wangu walijiona ni timu kubwa mbele Nsingizini Hotspurs, walicheza 'kifaza' na kuwadharau wapinzani.
"Matokeo ya mabao 3-0 ni mazuri, lakini hatukucheza kama tulivyopaswa kucheza, tunatakiwa kujiamini tunapokuwa na mpira," alisema kocha huyo ambaye ilikuwa mechi yake ya kwanza tangu alipoichukua timu kutoka kwa Fadlu Davids, ambaye kwa sasa ni kocha wa Raja Casablanca ya Morocco.
Alisema kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko, angalau aliona dalili ya kile ambacho anakitamani na kukitarajia kufanyika katika kikosi chake kwa siku zijazo anakapokuwa amepata muda wa kukaa na vijana wake kwa muda mrefu na kushiba mafunzo yake.
"Kipindi cha pili baada ya kuongea nao vijana, tulibadilika, tulifanya mabadiliko ya wachezaji, tulicheza vizuri kidogo licha ya kwamba uwanja ulikuwa umelowa na ulikuwa na barafu kutokana na mvua iliyokuwa inanyesha muda karibuni wote wa mchezo.
"Mechi ya marudiano kikubwa nitakachojaribu na kuongeza ubora kwenye uchezaji wa kikosi changu kwa sababu hata kama tutapita hapa, tutakwenda kukutana na timu ngumu zaidi ya hii," alisema Pantev.
Meneja huyo alishindwa kuficha furaha yake kutokana na kuwapo kwa mashabiki wengi wa Simba uwanjani hapo kiasi cha kudhani kwamba mechi hiyo inachezwa Tanzania.
Alisema kutokana na hilo, ameahidi kuwapa zawadi ya soka la burudani katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini ambapo mashabiki wataruhusiwa kuingia baada ya kumaliza kifungo cha kuzuiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
"Tunashukuru sana kwa sapoti yao, nimeshangaa hapa Eswatini walikuwa wengi sana, unaweza ukadhani labda tulikuwa tunacheza nyumbani, nadhani wengine watakuwa wametoka Tanzania, wengine kutoka nchi za jirani, ila nawaahidi zawadi yao wataipata Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mchezo safi ambao timu yao itautandaza, waje kwa wingi ili watupe nguvu na kuwanyong'onyesha wapinzani," alisema.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema mashabiki walioonekana uwanjani ni Watanzania walitoka katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe, Zambia, Angola, Botswana, Afrika Kusini na Eswatini yenyewe.
"Walikuwa ni zaidi ya 200, wao walisafiri kilometa nyingi na gharama nyingi za kusafiri pamoja na kuvuka mipaka, uongozi wa Simba ulichofanya ni kuwanunulia tiketi za kuingia uwanjani ili kuwashangilia wachezaji wetu," alisema Ahmed.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED