Pantev ataka wachezaji wote Simba kufunga mabao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:02 PM Nov 10 2025
news
Picha Mtandao
Meneja Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev.

MENEJA Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev, amesema mfumo anaoutumia kwenye kikosi hicho, unawapa nafasi wachezaji wake wote kufunga mabao, na hahitaji mastraika peke yake.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa juzi, Uwanja wa Meja Jenerali, Isamuhiyo, Mbweni, Dar es Salaam, timu yake ikishinda mabao 2-1, amesema  aina yake ya uchezaji wa kuwatumia mabeki wa kati kucheza pembeni zaidi ni kuwapa uwanda mpana wa kusaidia mashambulizi mbele, ikiwezekana kufunga mabao.

Dimitar anaonekana kupenda kutumia mabeki wa kati watatu nyuma, huku Wilson Nangu na Rushine De Reuck wakionekana kucheza pembeni zaidi.

Wakati Nangu alionekana zaidi upande wa kushoto, Rushine, huonekana upande wa kulia, huku viungo wa kati wakishuka chini wakati wao wanapokwenda mbele kusaidia viungo wengine eneo la kushambulia.

"Katika timu yangu nimetengeneza mfumo wa kwamba kila mchezaji afunge mabao, haijalishi ni beki, kiungo au mshambuliaji. Na hii inaonekana zaidi hasa kwenye faulo na kona kwa sababu nimeona wachezaji wangu wengi wana uwezo wa kutupia mpira ndani ya wavu," alisema.

Katika mchezo wa juzi, beki, Nangu, aliyesajiliwa msimu huu kutoka JKT Tanzania alifunga bao, likiwa la kwanza kwenye Ligi Kuu na la pili tangu ajiunge na timu hiyo.

Anakuwa beki wa kati wa tatu wa Simba kufunga bao kwenye Ligi Kuu, ambapo Rushine, raia wa Afrika Kusini ana mabao mawili mpaka sasa, Chamou Karaboue, raia wa Ivory Coast, akiwa pia na bao moja mpaka sasa.

Mabao yote waliyofunga mabeki hao yametokana na mipira iliyokufa, kona na faulo.

Akiuzungumzia mchezo wa juzi dhidi ya JKT Tanzania, alisema ni kweli haukuwa rahisi, lakini ugumu waliusababisha wenyewe kwa kukosa mabao mengi kipindi cha kwanza.

"Kila mechi kwetu kwenye Ligi Kuu itakuwa ngumu kwa sababu Simba ni timu kubwa, kila timu itataka kuja kucheza kwa nguvu kushindana nayo.

Hata hivyo, mechi hii tuliifanya ngumu wenyewe kwa sababu ya kukosa nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza, lakini niseme tu kuwa tulicheza vizuri," alisema.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ametamba kuwa wamewaangamiza JKT Tanzania kwa silaha zao wenyewe.

"Tumetumia silaha zao, tumeaangamiza JKT Tanzania kwa silaha walizotuuzia, tumetumia fedha nyingi kuwasajili, Yakoub Suleiman na Nangu, tulijua watakuja kuisaidia Simba, bila shaka mechi ya tatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kila mmoja ameona kwa nini tuling'ang'ana kuwasajili wachezaji hawa kwani haikuwa rahisi kwa JKT Tanzania kuwaruhusu kwani walikuwa ndiyo mhimili wao," alisema.

Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, alisema wachezaji wake walikosa umakini hasa baada ya kupata bao.

"Ukicheza na Simba lazima ujue hiyo mechi lazima iwe ngumu kwako. Tulipopata bao tuliondoa umakini, ambao wapinzani wetu walituadhibu. Kipindi cha kwanza tuliwadhibiti Simba, tulibadilika kipindi cha pili, ilibidi sasa tufunguke ili tupate bao, kweli ilikuwa hivyo, lakini tukaachia mianya, isingewezekana kucheza kwa kuzuia dakika zote 90, itakuwa haina maana kama unacheza kwa kuzuia tu bila kwenda mbele kupata bao," alisema.

Simba inakuwa timu pekee mpaka sasa kwenye Ligi Kuu kushinda kwa asilimia 100, ikifanya hivyo katika michezo yote mitatu iliyocheza, ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate na idadi kama hiyo ya mabao dhidi ya Namungo FC, ambapo sasa ipo kileleni na pointi tisa.

Kipigo hicho kinaifanya JKT Tanzania kupoteza mechi ya kwanza msimu huu, baada ya michezo mitano kupita bila kuacha pointi tatu, ikishinda moja na sare nne.