Rais Samia mgeni rasmi Bunge Bonanza

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:17 AM Jun 19 2025
Rais Samia mgeni rasmi  Bunge Bonanza
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Samia mgeni rasmi Bunge Bonanza

Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha kubwa la michezo na burudani la ‘Grand Bunge Bonanza’, linalotarajiwa kufanyika Juni 21, 2025 Jijini Dodoma.

Tamasha hilo litaambatana na matembezi maalum ya afya yatakayoanzia Chuo cha Mipango hadi viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlini, pamoja na tamasha la nyama choma, likiwa na lengo la kuhamasisha afya bora na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kupokea msaada wa vifaa vya michezo kutoka Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Timu ya Bunge Sports Club, Festo Sanga, amesema bonanza hilo linahitimisha mabonanza ya Bunge la 12, ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.

“Mwaka huu bonanza litakuwa la kipekee zaidi kwani linakuja siku chache kabla ya Bunge kufungwa rasmi na Rais. Tumeamua kuwa pamoja naye ili kuonesha mshikamano, umoja na kufunga pazia kwa pamoja,” amesema Sanga.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa benki hiyo, TullyEsther Mwampamba, amesema benki hiyo imetoa msaada wenye thamani ya Sh. milioni 130 kwa ajili ya michezo hiyo, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kupitia sekta za elimu, afya na michezo.

1