Michuano ya Umoja Cup Rorya 2025, imemalizika kwa Rorya United kutwaa ubingwa huo baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Masonga FC mabao 2-0, kwenye mchezo wa fainali uliopigwa juzi, Jumatatu.
Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Maji Sota wilayani hapa, mabao yote mawili ya Rorya United yalifungwa na Tizo Itera kipindi cha kwanza.
Michuano hiyo inayodhaminiwa na mdau na mpenda soka wilayani Rorya, Peter Owino, ilianza kutimua vumbi tangu Agosti 10, mwaka huu, huku jumla ya timu shiriki zikiwa 20.
Katika mechi hiyo ya juzi, Masonga FC iliyotinga fainali kwa kutoa kipigo cha mabao 2 - 0 dhidi ya Bubombi FC, haikuweza kufurukuta mbele ya Rorya United kwenye mchezo huo ulihudhuriwa na mashabiki wengi.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Rorya United imeondoka na kitita cha Sh. 600,000, jezi seti moja yenye thamani ya Sh. 224,000 na mpira wenye thamani ya Sh. 50,000/ pamoja na kombe lenye thamani ya Sh. 300,000.
Kwa upende wa Masonga FC imezawadiwa Sh. 400,000, jezi seti moja yenye thamani ya Sh. 224,000 na mpira wenye thamani ya Sh 50,000 huku mshindi wa tatu naye akipata zawadi kama hizo, lakini kwa upande wa fedha yeye akiondoka na Sh. 150,000.
Kwa upande wa mshindi wa nne ameabulia jezi seti moja yenye thamani ya Sh. 224,000 na mpira mmoja wenye thamani ya Sh. 50,000.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED