Simba Queens, Yanga Princess kuvaana Desemba 28

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:58 AM Nov 06 2025
news
Picha Mtandao
Simba Queens, Yanga Princess kuvaana Desemba 28, mwaka huu.

WATANI wa jadi, Simba Queens na Yanga Princess watakutana katika mechi ya mazunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania itakayofanyika Desemba 28, mwaka huu, imefahamika.

Mechi ya marudiano yenyewe itachezwa Aprili 23, mwakani.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imesema msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake sasa utaanza Novemba 14, mwaka huu badala ya leo kama ilivyotangazwa hapo awali.

Taarifa hiyo ilisema ratiba mpya iliyotolewa jana imezingatia Kalenda ya FIFA, mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026), zitakazofanyika Machi, mwakani.

Ratiba hiyo inayoonesha mechi zitakazofanyika siku ya ufunguzi zitakuwa ni kati ya Simba Queens dhidi ya Bilo Queens wakati Geita Gold Queens itawakaribisha Ceasiaa Queens huku Alliance Girls ikiwaalika Fountain Princess kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini, Mwanza.

Ruangwa Queens, timu mpya iliyopanda daraja wao watakuwa wenyeji wa Yanga Princess kwenye Uwanja wa Majaliwa huku Desemba 8, mwaka huu Mashujaa Queens itawafuata Tausi kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

“Kwa sababu ya majukumu ya kimataifa, JKT Queens wao watacheza mechi yao ya kwanza Desemba 8 dhidi ya Bunda Queens, tunaamini kila timu imejiandaa kuonesha ushindani katika msimu mpya,” Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, alisema jana.

Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika Mei 28, mwakani kwa timu zote 12 kushuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu.