SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), limesema zipo sababu mbalimbali zilizopelekea aliyekuwa Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, kupewa ‘mikoba’ ya kuifundisha Timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo inajiandaa kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), baadaye mwaka huu.
Juzi jioni TFF ilimtangaza Gamondi kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Stars kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho baada ya kuachana na Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Moja ya sababu hizo ni makocha waliopita akiwamo, Hemed Morocco, kwenda masomoni, pamoja na kubadilisha mawazo na mtazamo ndani kikosi hicho.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Ufundi wa (TFF), Oscar Milambo, amesema mabadiliko katika timu hiyo ni jambo la kawaida kwa sababu hata wachezaji wanakuja na kutoka kwenye kikosi hicho.
"Mshtuko lazima uwepo kwa mashabiki, lakini ni lazima kila mmoja afahamu hii na timu ya taifa, iko kama mbio za vijiti, watu kupokezana, walimu waliokuwapo mwanzo wamefanya kazi kubwa kwa sehemu yao, kwa sasa tunaangalia kama tunaweza kufanya vitu tofauti.
Mabadiliko ni lazima kwa watu tulionao, zipo sababu nyingi ambazo tunaweza tukazisema, moja ambayo ni muhimu ni kujaribu kubadilisha mtazamo wa timu ya taifa, mnaweza kuona wakati uliopita timu ilianzia wapi na ilikuwa wapi.
Gamondi ni kocha mwenye mashabiki wengi nchini, analifahamu soka la Tanzania na Ligi Kuu pia, amefundisha kwa kiwango cha hali ya juu, hivyo pamoja na ufundi wake, lakini anaweza kuwafanya mashabiki pia kuvutika kuja uwanjani kuona timu yao," alisema Mirambo.
Aliongeza TFF pia iko katika mchakato wa kumpeleka, Morocco na wasaidizi wake mafunzoni ili kulisaidia taifa hapo baadaye.
"Pia walimu ambao walikuwa katika kikosi chetu tuna plani ya kuwapeleka mafunzoni kuongeza elimu siku si nyingi, hivyo isingekuwa rahisi sana kuwatoa kwenye mazingira ya masomo wakati timu inatakiwa kujiandaa na mashindano. Huu ni uwekezaji, lazima tuwekeze kwa kuwaimarisha walimu wetu kwa ajili ya baadaye," Mirambo alisema.
Wakati huo huo, Singida Black Stars imempongeza Gamondi kwa kuteuliwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Stars.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo jana inasema uteuzi huo ni heshima kwao, pia ni uthibitisho wa ubora, taaluma na mafanikio ambayo Gamondi ameyaonesha tangu alipojiunga na kikosi hicho.
Klabu hiyo imesema itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha analeta matokeo chanya kwa Stars, sambamba na kuendeleza falsafa ya ushindani wakati akitekeleza majukumu ndani ya kikosi cha cha Singida.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED