Twiga Stars kuvaana na Malawi kesho

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 01:11 PM Oct 21 2025
news
Picha Shufaa Lyimo
Kocha Mkuu wa timu ya Twiga Stars Bakari Shime kushoto akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika mchezo wao wa kesho kulia ni Msemaji wa TFF Cliford Mario Ndimbo.

TIMU ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) kesho inatarajiwa kushuka dimbani majira ya saa 11:00 jioni kuumana na Ethiopia katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Wafcon 2026, mchezo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Chamanzi.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Kocha Mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime amesema maandalizi yamekamilika na kudai atamkosa mchezaji wake Winfrida Gerald ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu. Na kwamba fainali hizo zitafanyika nchini Morocco.  

"Ni mchezo muhimu kwetu naamini wachezaji wangu watafuata vizuri maelekezo niliyowapa ili tuweze kupata ushindi tukiwa nyumbani," amesema Shime. 

Amesema wapinzani hao watacheza nao wakifahamu Twiga Stars ipo juu kuliko wao na kuwataka watanzania wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yao. 

Amesema malengo yake ni kwenda kuandika historia kwa kuifunga Ethiopia, na kuweka wazi hali za wachezaji kiafya zinaendelea vizuri kwani hakuna majeruhi yoyote. 

Amesema wachezaji waliopo nje ya nchi bado wanaendelea kuripoti kambini ambapo mpaka kufika jana jioni wote walitarajiwa kuwepo kambini hapo kwa ajili ya mchezo. 

Nahodha wa timu hiyo Anastazia Katunzi amesema wapo tayari kuvaana na mpinzani wao huyo kutokana na maandalizi waliyoyafanya. 

"Tunatambua ni mchezo muhimu kwetu hivyo tutafuata vizuri maelekezo tuliyopewa na mwalimu wetu ili tuwape burudani watanzania," amesema Anastazia. 

Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Ethiopia Yosef Gebrewold alisema wataingia kwa tahadhari kwa kuwa wanatambua Twiga Stars ni miongoni mwa timu bora. 

"Kwa upande wetu tumejiandaa vizuri kukutana na Twiga Stars tunafahamu ina mashabiki wengi isipokuwa tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo ugenini," amesema Gebrewold.