MABINGWA watetezi wamesema wako tayari kuondoka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam ili kuendeleza mbio za kulibakisha taji hilo Jangwani.
Katika mchezo huo, wanachama na mashabiki wa Yanga wanatarajia kumwona kwa mara ya kwanza mchezaji wao mpya, Jonathan Ikangalombo, ambaye hakupata nafasi kwenye mchezo uliopita wa michuano ya Kombe la FA, dhidi ya Copco.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga, Walter Harrison, alisema ni muhimu kwao kushinda mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili ili kukiongezea nguvu kikosi chao kuelekea katika vita ya kutwaa ubingwa.
Akizungumza baada ya mazoezi ya jana asubuhi, Walter, alisema wanataka kuanza mzunguko wa pili kwa ushindi ili kuendeleza mbio za kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo msimu huu zimeonekana kuwa na kasi ya aina yake.
"Mchezo dhidi ya Kagera Sugar ni muhimu sana, kwa sababu malengo yetu yaliyosalia ni kubakisha taji letu la Ligi Kuu, Kombe la FA, kila kitu kinakwenda kwa mtiririko huu. Tumekuwa na maandalizi mazuri, kila kitu kinaenda sawa, kikosi kimetimia, kila mchezaji anaweza kuwa sehemu ya kikosi hicho, ukiondoa Yao Kouassi, ambaye amefanyiwa upasuaji.
Tunajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na timu nyingi katika mzunguko huu zimefanya usajili, na kila mchezaji atajitahidi kucheza kwa nguvu ili kuwaaminisha walimu wao yuko sawa kwa ajili ya kusaka namba, lakini sisi Yanga tumejiandaa kukabiliana na yote, tuko sawa kuivaa Kagera Sugar na kupata ushindi pia," alisema meneja huyo.
Yanga itaingia katika mchezo huu, ikiwa ni wiki moja tu baada ya kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Copco na kutinga hatua ya 32 Bora ya mashindano ya Kombe la FA.
Katika uwanja wa mazoezi jana, Kocha Mkuu, Sead Ramovic, alionekana kuwapa zaidi wachezaji wake mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili pamoja na kasi.
Mbali na Ikangalambo ambaye hakucheza mechi dhidi ya Copco, kutokana na kupatwa na homa ya ghafla, iliyomfanya asiwe kwenye mipango yake Ramovic, kesho huenda Israel Mwenda, ambaye alicheza mechi iliyopita kwa mara ya kwanza, na akatoa pasi mbili zilizozaa mabao, ataitumikia Yanga katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga yenye pointi 39 iko kwenye nafasi ya pili nyuma ya vinara, Simba yenye pointi 40.
KenGold FC ya jijini, Mbeya ambayo juzi iliwatambulisha nyota wake wapya akiwamo winga, Bernard Morrison, inaburuza mkia ikiwa na pointi sita kibindoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED