WAKATI ikisema imepangwa katika kundi la ‘kifo’ katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imetangaza rasmi kutumia Uwanja wa New Amaan Complex ulioko Zanzibar katika michezo yake ya hatua ya makundi.
Yanga imepangwa Kundi B pamoja na Al Ahly ya Misri, AS FAR (Morocco) na JS Kabylie ya Algeria na itaanzia hatua hiyo kwenye uwanja wa nyumbani.
Akizungumza na gazeti hili jijini, Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema uongozi wa klabu hiyo umeamua kuzipeleka mechi zao Zanzibar kwa ajili ya kuzingatia maslahi ya timu hiyo.
Kamwe alisema wanaamini Yanga itakuwa na wakati mzuri visiwani humo na baada ya kumaliza michezo mitatu ya hatua hiyo watatoa taarifa nyingine endapo watafanikiwa kusonga mbele.
"Kuelekea katika mechi hizi za hatua ya makundi, baada ya kufanya tathimini ya kina na kwa kuzingatia maslahi mapana ya klabu yetu, niwatangazie wanachama, mashabiki wa Yanga na wapenzi wa soka wote nchini, mechi zetu za hatua ya makundi zitafanyika Visiwani, Zanzibar, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, baada ya hapo kama tukimaliza na kama tumevuka, kuna utaratibu mwingine tutawatangazia.
Ratiba inaonesha tutaanzia nyumbani dhidi ya AS FAR ya Morocco, baada ya hapo tutasafiri kwenda Algeria kucheza na JS Kabylie, halafu tutakuwa tena ugenini dhidi ya Al Ahly (Misri) halafu tutageuza nao kuja kucheza nao hapa (New Amaan Complex), tukimalizana nao tutasafiri kwenda kurudiana na AS FAR ugenini, halafu mchezo wetu wa mwisho tutamalizia nyumbani dhidi ya JS Kabylie," alisema Kamwe.
Ofisa huyo alikiri kwa kutaja kundi ambalo wamepangwa ni gumu kutokana na aina ya timu zilizopo pamoja na ubora wa ligi wanazoshiriki kwenye nchi husika.
"Majuzi ilifanyika droo na timu yetu imeangukia Kundi B. Ukiangalia hili kundi, kila mmoja ambaye anajua mpira na anafuatilia masuala ya soka la Afrika atakiri hili ndiyo kundi gumu, kundi la kifo kwa sababu ya ubora wa timu zote nne, pia inahusisha timu zilizotoka Ligi Bora Afrika.
Utaona hapo kuna Ligi ya Misri, Morocco, Algeria na Tanzania, siyo kundi jepesi wala lelemama, sisi kama viongozi tunakiri hivyo na kusema halitabiriki, yoyote anaweza kupata nafasi ya kusonga mbele. Tutaanza mipango kuhakikisha sisi ni moja ya timu mbili zitakazopita hatua hiyo," Kamwe alisema.
Aliongeza kikosi cha timu hiyo tayari kimerejea kambini jana kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC, utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Yanga imesema straika wake, Clement Mzize, amefanyiwa upasuaji wa goti.
Kamwe aliliambia gazeti hili upasuaji huo umefanyika baada ya ushauri wa jopo la madaktari, benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe.
"Baada ya vipimo na ushauri wa madaktari, benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe, tukaamua kuafiki mchezaji huyo akafanyie upasuaji.
Kwa sababu alikuwa anapona, lakini akirudi tena uwanjani anaumia, sasa baada ya kufanyika uchunguzi kwa kina, tukaamua akafanyie operesheni ya sehemu ya goti.
Ninavyozungumza na nyinyi, upasuaji umefanyika na mchezaji anaendelea vizuri. Tutamkosa Mzize kwa kipindi cha wiki nane mpaka 10 kwa mujibu wa jopo la madaktari lilivyoelekeza," alisema Ofisa habari huyo.
Kufuatia upasuaji huo, Mzize, ataikosa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyobakia mwaka huu, mechi za hatua ya makundi za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), zitakazofanyika kuanzia Desemba 21, mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED