KLABU ya Yanga imekiri kuwapo kwa ugumu wa kupata matokeo ya ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu msimu huu tofauti na misimu kadhaa iliyopita, huku ikifurahia kukaa kileleni mwa msimamo mpaka sasa.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema jana kwa michezo minne ambayo timu yao imecheza, imewapa picha kuwa wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kupata ushindi katika kila mchezo, pia kufikia mafanikio ya msimu uliopita kutokana na kuwapo kwa ubora wa timu nyingi kwenye Ligi Kuu kwa sasa.
"Tumecheza michezo minne mpaka sasa, ni mapema sana kuzungumza nini kitakwenda kutokea mwisho wa msimu, lakini kwa michezo hii tu inatupa ligi ni ngumu sana msimu huu, tunatakiwa tupambane zaidi msimu huu kuliko uliopita au mingine ili tuweze kupata matokeo mengi mazuri kama si kuifikia, basi tuipiku rekodi ya msimu uliopita, si kazi rahisi, lakini tutapambana," alisema Kamwe.
Yanga imecheza michezo minne ya Ligi Kuu mpaka sasa, ikishinda mitatu na kutoka sare mmoja. Iliifunga Pamba Jiji mabao 3-0, Mtibwa Sugar 2-0, KMC FC 4-1, ambapo ililazimishwa suluhu dhidi ya Mbeya City, hivyo kukusanya pointi 10 mpaka sasa.
"Ligi imeanza vizuri, kumekuwa na ushindani mkubwa na hamasa pia, lakini hivi tunavyozungumza sasa Yanga ndiyo vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi mpaka sasa, na kuruhusu machache, kwa ugumu jinsi ulivyo tunafurahia kukaa kileleni," alisema Ofisa Habari huyo.
Yanga imefunga mabao tisa mpaka sasa, ikiwa inaongoza kwa kupachika mabao mengi ikifuatiwa na Simba yenye mabao manane.
Timu hiyo imeruhusu bao moja tu mpaka sasa katika michezo minne iliyocheza, ikiwa sawa na Simba iliyoshuka dimbani mara tatu tu na Singida Black Stars ambazo zote zimeruhusu bao moja pia.
Kamwe pia ametangaza kuwa klabu hiyo leo itazindua jezi ambazo itakwenda kuzivaa katika mechi za kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mikakati ya kuivaa AS FAR ya Morocco, katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi, utakaopigwa, Novemba 22, mwaka huu, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
"Kuanzia uongozi mpaka benchi la ufunfi, tayari tumeanza mikakati yetu kuelekea mchezo wetu wa kwanza hatua ya makundi, wanachama waendelee kufuatilia utaratibu tutakaoutoa kuelekea kwenye hamasa ya timu yetu, tunajipanga kisawasawa ili kuanza vizuri kwenye kundi letu," alisema Kamwe.
Aidha, amesema hawatakuwa tayari kupoteza mchezo wao wa kwanza hatua hiyo tena wakiwa nyumbani.
"Kwanza niwaombe mashabiki na wanachama wa Yanga, wajiandae twende kuujaza Uwanja wa New Amaan, wachezaji wetu na benchi la ufundi wanapambana na maandalizi ili kuwapa Watanzania furaha siku hiyo, hivyo sisi mashabiki tusibaki nyuma, tujitokeze kwa wingi siku ya mchezo, utaratibu wote tutaitoa," alisema Kamwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED