WAKATI klabu ya Yanga ikimtambulisha kocha wake mpya, Pedro Goncalves mwenye umri wa miaka 49, raia wa Ureno usiku wa kuamkia jana, Kaimu Kocha, Patrick Mabedi amesema ushindi walioupata juzi dhidi ya Silver Strikers kwa kiasi kikubwa unatokana na yeye kuwafahamu wachezaji wa timu hiyo ya Malawi.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza wa ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa juzi jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mabedi alisema kwa sababu yeye alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Malawi, amewafundisha wachezaji wengi wa Silver Strikers ambao asilimia kubwa ndiyo wanaounda kikosi cha timu hiyo.
Alisema alichofanya ni kuainisha aina ya uchezaji, tabia na mikimbio yake, uhatari na udhaifu na kuufanyia kazi kwa wachezaji wa Yanga ambao waliweza kuwamudu na kupata ushindi wa mabao 2-0.
"Wachezaji wengi wa timu ya Silva wanaichezea pia timu ya taifa ya Malawi, mimi nilikuwa kocha wao kwa hiyo nawafahamu sana na hii ilikuwa faida kubwa kwetu kuchukua taarifa zao, aina yao ya uchezaji na kuufanyia kazi. Tulicheza tukijua tabia zao, mikimbio yao uwanjani, kila mmoja ni hatari akiwa wapi na udhaifu, kazi tuliyoifanya ni kuwadhibiti kwa kutumia faida ya kuwafahamu kwangu, nikawaambia wachezaji jinsi gani ya kucheza nao na kweli mpango kazi umefanikiwa," alisema Mabedi.
Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo huo na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 2-1.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Bingu Mutharika, Malawi, Jumamosi iliyopita, Yanga ilifungwa bao 1-0.
Kocha huyo aliwashukuru wanachama na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao, ambapo wingi wao umekuwa na faida ya kuisaidia kuipeleka Yanga hatua ya makundi kutokana na sapoti yao.
"Haikuwa mechi rahisi, tulifanya vitu vya msingi, tuna wachezaji wenye vipaji na viwango vikubwa, tulichotakiwa ni kutumia nafasi na tumefanya hivyo dakika za mwanzo na kutuweka mchezoni. Tunashukuru kwa mashabiki kuja kwa wingi uwanjani nayo imetusaidia sana," alisema Mabedi ambaye aliiongoza timu hiyo kama kaimu kocha mkuu, baada ya kutimuliwa kwa Romain Folz, muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Malawi.
Inakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwa Yanga kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa ni mara ya nne kwenye historia ya timu hiyo.
Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1998 pamoja na msimu miwili mfululizo.
Katika misimu yote hiyo, mara mbili iliishia hatua ya makundi, ukiwamo msimu uliopita, ikifika robo fainali msimu mmoja, ikitolewa dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti.
Wakati huo huo, Yanga ilimtambulisha kocha mpya Pedro ambaye ndiye atakuwa Kocha Mkuu, akichukua nafasi ya Folz.
Pedro amewahi kufundisha klabu ya Sporting Lisbon, De Agosto na timu ya taifa ya Angola.
Rekodi kubwa na bora ya kocha Pedro ni kuifikisha timu ya Taifa ya Angola hatua ya robo fainali kwenye michuano ya mataifa ya Afrika, AFCON, iliyofanyika nchini Ivory Coast.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED