STRAIKA Mkongomani, Andy Boyeli aliyesajiliwa msimu huu kutoka Sekhukhune ya Afrika Kusini, jana alifunga mabao mawili, akiwaongoza Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kuwafumua KMC, mabao 4-1, katika mchezo wa Ligi Kuu, uliochezwa, Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Ulikuwa mchezo wa 12 kwa Yanga tangu zilipoanza kukutana msimu wa 2018/19, zikicheza mara 15, zikitoka sare mbili, huku KMC ikipata ushindi mara moja tu, mechi iliyochezwa Machi 12, 2020, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, msimu wa 2019/20, ikishinda bao 1-0, lililofungwa na Salim Aiyee.
Boyeli, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Prince Dube, alipachika bao dakika ya 81 kwa mkwaju wa penalti, baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari, lilikuwa bao la tatu kwenye mchezo huo.
Dakika za majeruhi, aliukwamisha mpira wavuni, akimalizia pasi murua ya Celestin Ecua, aliyeingia kuchukua nafasi ya Mohamed Doumbia.
Kabla ya hapo, Yanga ilipata bao la kwanza, lililofungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 36 kwa shuti la karibu, akimalizia pasi mpenyezo kutoka kwa Pacome Zouzoua.
Bao hilo lilitokana na Yanga kuliandama lango la KMC kwa muda mrefu wa mchezo, lakini mabeki wa timu hiyo walikaa imara, kabla ya kufanya kosa hilo lililozaa bao.
Lilikuwa ni bao la pili kwa mchezaji huyo Mkongomani kwenye Ligi Kuu hadi sasa.
Daruweshi Saliboko, aliisawazisha KMC bao, dakika tatu kabla ya mapumziko, alipoukimbilia mpira uliotemwa na kipa Diarra.
Ilikuwa ni faulo iliyopigwa na Chambo ambayo ilitemwa na Diarra, Saliboko alichomoka kwa kasi, akauwahi mpira na kuachia shuti kali lililokwenda kushoto kwa kipa huyo na kujaa wavuni.
Linakuwa ni bao la pili kwa straika huyo wa KMC.
Wakati mashabiki wa Yanga wakiwa na wasiwasi wa timu yao ikiwa sare, Pacome alifunga bao la pili dakika ya 72 kirahisi, baada ya krosi ya Israel Mwenda kuwapita mabeki wa KMC na kumkuta mfungaji aliyeupachika wavuni, likiwa ni bao lake la kwanza msimu huu kwenye Ligi.
Yanga jana imeruhusu bao kwa mara ya kwanza baada ya kucheza mechi tisa, michezo nane ikiwa haijaruhusu bao.
Mara ya mwisho ilikuwa Aprili 10, mwaka huu Ligi Kuu msimu uliopita, iliporuhusu bao dhidi ya Azam FC, mechi ambayo ilitoka na ushindi wa mabao 2-1.
Kipa wa Yanga, Diarra, jana aliruhusu bao na kukosa 'clean sheets' baada ya michezo mitatu.
Yanga imefikisha pointi 10 na kukaa kileleni mwa msimamo, ikiwa imecheza michezo minne, wakati Simba iliyoshinda juzi dhidi ya JKT Tanzania, mabao 2-1, ikishika nafasi ya pili, ikiwa na pointi tisa, baada ya kucheza michezo mitatu.
KMC, ilipata kipigo cha tano mfululizo, ikiendelea kukamata mkia ikiwa na pointi tatu.
Timu hiyo ilishinda mchezo mmoja tu kwa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Septemba 17 mwaka huu, baada ya hapo imepoteza michezo yake yote iliyofuata.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED